Uchaguzi wa kwanza wa urais tangu kifo cha deby itno kufanyika mei 6 chad

Tume ya uchaguzi ya Chad imesema duru ya kwanza ya uchaguzi wa rais itafanyika tarehe 6 Mei.

Kura hizo za maoni zitaashiria mwisho wa kipindi kirefu cha mpito cha kijeshi ambacho kilianza mwaka 2021 baada ya kifo cha kiongozi wa muda mrefu Idriss Deby Itno.

Kulingana na kalenda ya uchaguzi iliyochapishwa Jumanne, duru ya pili ya upigaji kura itaandaliwa mnamo Juni, na matokeo ya mwisho yanatarajiwa Julai.


Rais wa tume ya uchaguzi, Ahmet Bartchiret alisema ilikuwa ni lazima uchaguzi ufanyike kabla ya Oktoba 10, tarehe ambayo kipindi cha mpito cha kijeshi kinafaa kumalizika.

Mahamat Idriss Deby amekuwa akiongoza nchi kwa karibu miaka mitatu sasa, licha ya ahadi ya awali ya kuondoka baada ya kipindi cha mpito cha miezi 18.

Kipindi cha mpito kiliongezwa baadaye kwa miaka miwili, na hivyo kurefusha kukaa kwake madarakani.

Mwezi uliopita, Chama cha Patriotic Salvation Movement (MPS) kilimtaja Deby kama mgombeaji wake katika uchaguzi wa urais, lakini bado hajatoa maoni yake rasmi kuhusu iwapo atagombea.

Katiba mpya iliyopiga kura mwezi Disemba inamruhusu kusimama kama mgombea, na kuzua maswali kuhusu ahadi ya kukomesha utawala wa kijeshi.

Share: