Tuyaenzi na kuyalinda mapinduzi matukufu ya zanzibar - dkt.biteko

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko ametoa wito kwa Wananchi kuendelea kuyaenzi, kuyalinda na kuyaishi kwa dhamira ya dhati, Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwani Waasisi wa Nchi walifanya mapinduzi hayo ili kuwa na Taifa huru ambalo kila mtu anakuwa na hadhi, kuondoa dhuluma iliyokuwepo na kufanya wananchi kuishi kwa amani na furaha.

Amesema hayo tarehe 6 Januari 2024 wakati akizungumza na Wananchi katika Wilaya ya Mkoani, mkoani Kusini Pemba mara baada ya kuzindua Afisi ya Uhamiaji na Makaazi ya Askari wilayani humo.

“ Sisi Wananchi tunawajibu wa kuyaenzi Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar kwa kuyaishi, kuyaheshimu, kukuza uchumi wa nchi na kukuza uzalendo ili baada ya muda mrefu hata baada ya miaka 100 mbele, watakaokuja kusherehekea Mapinduzi haya wakute Zanzibar iliyobora zaidi na waseme Mapinduzi haya yalitufaa.” Amesema Dkt. Biteko

Ameeleza kuwa, moja ya tunu tuliyonayo ni mshikamano hivyo watu wasiruhusu mtu yoyote kuwagawanya kwa misingi yoyote ile, bali maendeleo yaunganishe watu wote na kwamba tofauti za vyama, dini na kabila visifanye watu wakae kwenye makundi bali kuunganisha watu kwa maslahi ya nchi na watanzania.

Amesema kuwa, nchi inapoenda kusherehekea Siku ya Mapinduzi ya Zanzibar tarehe 12 Januari mwaka huu, watanzania wote waungane kuwaombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt, Samia Suluhu Hassan na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi, ili waendelee kuongoza vyema, kuimarisha ustawi wa Taifa na kuwaunganisha Watanzania.

Kuhusu Jengo hilo jipya la Afisi ya Uhamiaji katika Wilaya ya Mkoani, mkoani Kusini Pemba, Dkt, Biteko amesema kuwa ni moja ya matunda ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964 kwani kabla ya Mapinduzi watu walinyimwa haki zao za kimsingi zikiwemo za uhamiaji kama vile kupata pasi ya kusafiria na hivyo Mapinduzi yamewezesha wananchi kupata uhuru wa kusafiri nje ya mipaka ya nchi.

Ameongeza kuwa, Ofisi hiyo ya Uhamiaji wilaya ya Mkoani ilianza mwaka 1979 ikiwa ni ndogo lakini sasa kuna jengo la kisasa litakalowezesha upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi wa Wilaya hiyo na viunga vyake, ikiwa ni kielelezo cha Mafanikio ya Mapinduzi ya Zanzibar.







Share: