Tutaendelea kuenzi mazuri ya hayati lowassa - rc makonda

Enzi za uhai wake Hayati Edward Ngoyai Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kati ya Mwaka 2005-2008

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda amewaahidi wakazi wa Monduli kwamba Serikali ya Mkoa itahakikisha inatimiza maono ya Waziri Mkuu mstaafu Hayati Edward Ngoyai Lowassa aliyefariki dunia Februari 10, 2024 wakati akipatiwa matibabu kwenye Taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete.


Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Christian Makonda ametoa ahadi hiyo mapema leo Mei 27, 2024 wakati alipofika Kijijini Monduli, nyumbani kwa Hayati Edward Ngoyai Lowassa na kuzuru kaburi lake kumuombea kheri na pumziko jema wakati akiendelea na ziara ya kukagua miradi ya maendeleo wilayani humo.

Mhe. Paul Christian Makonda ameiombea familia ya Waziri Mkuu huyo kuwa Mwenyenzi Mungu aendelee kuwapa subira, uvumilivu na kuwajalia mwanzo mpya wa maisha bila ya Mzee Lowassa, akimtaja kama kiongozi aliyeacha alama nyingi kwa wana Arusha na Watanzania wote kwa Ujumla.

Mhe. Paul Christian Makonda amemtaja Hayati Edward Ngoyai Lowassa kama kiongozi mwenye uthubutu na uchapakazi wa hali ya juu kwenye nafasi zake mbalimbali alizowahi kuzitumikia, akiwa pia kiongozi mwenye kusimamia alichokiamini mara zote katika kipindi cha uhai wake.


"Uthubutu wake ukawe alama na kumbukumbu ya kutosha katika kuwapigania wananchi hasa wanyonge bila kujali gharama inayoweza kutokea katika mapambano ya kudai haki", ameongeza Mhe. Paul Makonda.

Enzi za uhai wake Hayati Edward Ngoyai Lowassa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Tanzania kati ya Mwaka 2005-2008, anakumbukwa na Watanzania wengi katika maono yake ya kukuza elimu kwa watoto wa maskini ili kupambana na umaskini, haki ya maji safi na salama kwa watanzania wote pamoja na kukuza demokrasia nchini Tanzania.

Share: