Tanzania imeshiriki kwa mafanikio makubwa katika Maonesho ya Kimataifa ya Utalii ya Japan (Japan Tourism EXPO 2023), yaliyofanyika kuanzia tarehe 26 - 29 Oktoba 2023 Jijini Osaka, Japan.
Maonesho hayo, yamekuwa ya kwanza kufanyika katika jiji hilo baada ya janga la UVIKO – 19 na yameshirikisha takriban makampuni ya watalii 1,275 kutoka nchi zipatazo 70 duniani.
Katika ufunguzi wa Maonesho hayo, Balozi wa Tanzania nchini Japan, Mheshimiwa Baraka Luvanda aliinadi Tanzania kuwa ni nchi yenye vivutio mbalimbali vya utalii hususan, Ngorongoro, Serengeti, Kilimanjaro na Zanzibar.
Kadhalika, Balozi Luvanda aliwataka mawakala wa utalii wa Japan waliojumuika na mawakala wa Tanzania kuchangamkia fursa mbalimbali za utalii. Aidha, alifanya mazungumzo na Kamishna wa Taasisi ya Utalii ya Japan kuhusu fursa mbalimbali za uwekezaji kwenye sekta ya utalii, kwenye mikutano ya pembezoni mwa Maonesho hayo.
Balozi Luvanda alitumia fursa hiyo kuelezea Maonesho ya Utalii ya Kimataifa ya Swahili (Swahili Internation Tourism Expo – S!TE) ya mwaka 2024 yatakayofanyika nchini mwezi Oktoba 2024 ambapo wadau mbalimbali wa utalii wa Japan wamehamasika kujiandikisha ili waweze kushiriki kwa lengo la kujiunganisha kibiashara na mawakala wa utalii wa Tanzania.