Tanzania yapiga hatua utekelezaji wa ajenda ya afrika 2063, asema dkt. biteko

Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika itaendelea kutekeleza, kusimamia,na kuendeleza harakati hizi za kuifanya Ajenda hii kutimiza Dira ya Afrika tuitakayo.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko kwenye Mkutano wa kujadili utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa na Wakuu wa Nchi juu ya Ajenda 2063 kwa nchi za Afrika, alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye mkutano huo jijini Gaborone, Botswana, ulioenda sambamba na maadhimisho ya Tamasha la KUSI.

Dkt Biteko alisema kuwa, kimsingi Tanzania imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa Ajenda hiyo ikiwemo masuala ya amani, usalama na demokrasia kupewa kipaumbele kwenye nchi, kuunganisha miradi mbalimbali ya maendeleo na nchi za Afrika ikiwemo ule wa SGR, pamoja na miradi ya umeme kupitia nchi za Kenya, Uganda, Ethiopia, na Zambia, na kufungua fursa za kiuchumi kwa nchi za Afrika. 

"Tanzania kama ilivyo kwa nchi nyingine za Afrika itaendelea kutekeleza, kusimamia,na kuendeleza harakati hizi za kuifanya Ajenda hii kutimiza Dira ya Afrika tuitakayo. " Alisisitiza Mhe. Dkt. Biteko

Ajenda ya Afrika 2063 Afrika tuitakayo imebeba vipaumbele Saba ambavyo ni pamoja na kuleta Afrika pamoja kwenye masuala ya Maendeleo, kuunganisha Bara la Afrika kwenye masuala ya kisiasa kwa kutumia tunu za Afrika, Utawala Bora na unaozingatia sheria, Demokrasia, na Haki, Kuilinda Afrika, Afrika yenye mwelekeo wa utamaduni wake na Maadili, Afrika itakayowaletea Maendeleo watu wake, kwa manufaa ya wanachi wa Afrika. 

Aidha Mhe Dkt. Biteko alishiriki mjadala wa Marais kutoka Afrika kuhusu Ajenda ya umoja wa Afrika 2063 ijulikanayo kama Africas Agenda 2063 inayotoa mwelekeo wa Afrika kutimiza ndoto zake na kuifanya Afrika waitakayo, mjadala uliohusisha Rais wa Jamhuri ya Watu wa Botswana, Mhe. Dkt. Mokgweetsi Masisi, Rais wa Zimbabwe Mhe. Emmerson Mnangagwa, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Rwanda Mhe. Dkt. Edouard Ngirente akimwakilisha Mhe. Rais, Paul Kagame, na Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Doto Biteko, akimwakilisha Mhe. Dkt Samia suluhu Hassan. 

Katika mjadala huo Mhe. Dkt. Biteko Alitoa tathmini ya utekelezaji wa Malengo ya Ajenda ya Afrika 2063 na tathmini ya miaka kumi ya awali kwa Tanzania, ambapo alisema kuwa Tanzania iliridhia mikataba ya utekelezaji wa Ajenda hiyo ya Afrika mwaka 2013 katika utekelezaji wa dira hiyo ya Afrika ambapo imepiga hatua kubwa katika uanzishwaji wa eneo huru la Biashara la Afrika na kuondoa vikwazo vya kibiashara, watu na bidhaa kwa maendeleo ya Tanzania.

Aidha, Mhe Dkt. Doto Biteko akiwa nchini Botswana alipata fursa ya kukutana na Rais wa Botswana na kuwasilisha salamu rasmi kutoka kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania . Dkt. Samia Suluhu Hassan ambapo pamoja na masuala mengine walijadili namna watakavyoboresha uhusiano na ushirikiano kati ya nchi hizo mbili ikiwemo kuangalia uwezekano wa kufungua ubalozi nchini Botswana ili kurahisisha utendaji kazi, ushirikiano kwenye masuala ya kiuchumi, Madini, Sanaa, na Utamaduni. 

Ujumbe wa Tanzania ulioongozana na Mhe. Dkt Biteko ni pamoja na Waziri wa Nchi ofisi ya Rais anayeshughulikia Kazi, Uchumi na Uwekezaji kutoka Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Mhe. Mudrick Soragha, Mkurugenzi wa Mipango kutoka Tume ya Mipango, Dkt. Mursali Ally Milanzi, Mkurugenzi Msaidizi anayeshughulikia masuala ya Afrika kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bi Ellen Maduhu pamoja na Balozi Edward Komba, Mkuu wa Utawala na Kaimu Balozi wa Tanzania Pretoria na anayeshughulikia Botswana.

Share: