Tanzania ina takriban hekta milioni 48.1 za rasilimali za misitu, sawa na asilimia 55 ya ardhi yote ya Tanzania Bara ambayo ikitumika vizuri kupitia miradi ya biashara ya kaboni ni suluhisho muhimu la kupunguza kasi ya uharibifu na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa.
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imeweka milango wazi kwa wawekezaji nchini na duniani kote kuwekeza kwenye biashara ya hewa ukaa ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa "Ibara ya 6.4" ya Mkataba wa PARIS, ambayo inalenga kukabiliana na kupunguza athari za mabadiliko ya tabia ya nchi duniani kote.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) katika mkutano wa kutatua changamoto za mabadililiko ya tabia nchi kwa kuongeza matumizi ya Masuluhisho Asilia uliofanyika leo Novemba 16, 2023 jijini Dar es Salaam.
”Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake imefungua milango na kuwakaribisha wote wenye nia ya kuwekeza katika biashara ya kaboni nchini Tanzania” amesisitiza Mhe. Kairuki.
Amesema Tanzania ina takriban hekta milioni 48.1 za rasilimali za misitu, sawa na asilimia 55 ya ardhi yote ya Tanzania Bara ambayo ikitumika vizuri kupitia miradi ya biashara ya kaboni ni suluhisho muhimu la kupunguza kasi ya uharibifu na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa. Amesema fursa hii kubwa pamoja na fursa nyingine kama vile ardhi oevu nk vinaweza kutoa faida zaidi katika ufadhili wa kaboni kwa wawekezaji wa ndani
Akiongelea faida ambazo Tanzania imezipata kutokana na biashara ya hewa ukaa, Mhe. Kairuki amesema mpaka sasa vijiji vinane (8) vya Wilaya ya Tanganyika vimepokea zaidi ya TZS bilioni nane katika kipindi cha miaka mitano (5) iliyopita chini ya msaada wa Kampuni ya Carbon Tanzania na Kampuni hiyo iko mbioni kushirikisha maeneo matano (5) ya usimamizi wa wanyamapori - WMA yaliyoko Kusini mwa Tanzania.