Tahadhari za kiafya katika kipindi cha mvua kubwa.

Kutokana na Mvua za vuli na masika zinazoendelea hapa nchini ,wito umetolewa kwa wananchi kuendelea kuchukua tahadhari za kiafya ikiwemo kudumisha usafi wa mazingira katika maeneo yao ili kuzuia magonjwa ya mlipuko.

Wito huo umetolewa Jijini Dodoma na Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma, Wizara ya Afya Dkt. Tumaini Haonga ambapo amesema mvua zinaponyesha kuna uwezekano wa athari za afya zinazoweza kujitokeza ikiwemo uharibifu wa miundombinu ya majitaka hali inayoweza kusababisha kusambaa kwa magonjwa ya mlipuko.

“Kutokana na Mvua zinazoendelea kunyesha,kuna athari za kiafya zinazoweza kujitokeza ikiwemo uharibifu wa miundombinu ya majitaka ambayo yanaweza kuchangia au kuibua kusambaa kwa magonjwa ya mlipuko kama vile ugonjwa wa Kipindupindu lakini kuongezeka kwa magonjwa yanayosababishwa na minyoo, homa ya matumbo, kwa hiyo nitumie fursa hii kutoa wito kwa wananchi wenzangu na jamii kwa ujumla kwa kipindi hiki mvua zinaendelea katika maeneo mbalimbali wazingatie kanuni za afya kwa kudumisha usafi wa mazingira na kuepusha maji kutuama kwenye maeneo ya makazi”amesema.

Ikumbukwe kuwa kutokana na utabiri wa hali ya hewa uliotolewa na Mamlakaya Hali ya Hewa nchini,uwezekano wa kuwepo kwa Mvua juu ya Wastani uwepo wa El Nino kuanzia sasa hadi Januari 2024 hasa katika mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara, Kigoma, Morogoro, Pwani , Dar Es Salaam, Tanga, Arusha, Manyara, na Kilimanjaro, Wizara ya Afya imekuwa mstari wa mbele kutoa elimu ya afya ikiwemo wazazi na walezi kuwa makini na watoto kipindi chote ambacho mvua zitakuwa zinanyesha, watoto kutoruhusiwa kucheza kwenye mvua au maji na kutocheza kwenye kingo za mito kwani kuna uwezekano wa kubomoka na kusababisha mtu kuteleza na kusombwa na maji.

Share: