Bi Mapisa-Nqakula anashtakiwa kwa madai kadhaa ya kuitisha hongo ya kiasi cha dola 120,000
Spika wa Bunge la Afrika Kusini Nosiviwe Mapisa-Nqakula amejiuzulu baada ya polisi kuvamia nyumba yake wakati wa uchunguzi wa rushwa.
Bi Mapisa-Nqakula anadaiwa kuomba hongo ili kupeana kandarasi wakati alipokuwa waziri wa ulinzi.
Amekana mashtaka na kusema kujiuzulu kwake "hakukuwa dalili au kukubali hatia".
Alisema kutokana na "uzito" wa uchunguzi hawezi kuendelea na jukumu lake.
Bi Mapisa-Nqakula mwenye umri wa miaka 67 na mpambanaji dhidi ya ubaguzi wa rangi aliteuliwa kuwa spika mwaka wa 2021. Kabla ya hapo, alihudumu kama waziri wa ulinzi kwa miaka saba.
Wiki iliyopita mawakili wa Mapisa-Nqakula waliwasilisha ombi la kutaka amri ya mahakama izuie kukamatwa kwake, wakisema ingevunjia heshima yake.
Siku ya Jumanne, majaji walikataa ombi hilo kwa msingi kwamba suala hilo halikuwa la dharura na hawakuweza kukisia juu ya kukamatwa ambako bado hakujafanyika.
Bi Mapisa-Nqakula anashtakiwa kwa madai kadhaa ya kuitisha hongo ya kiasi cha dola 120,000, kutoka kwa mmiliki wa kampuni ili kupata zabuni ya kusafirisha vifaa vya jeshi nchini Afrika Kusini kutoka kwingineko barani, gazeti la Business Day linaripoti. .
Kujiuzulu kwakekunajiri kabla ya uchaguzi mkuu wa mwezi ujao, ambao baadhi wanaamini unaweza kuwa mgumu kwa chama tawala cha African National Congress (ANC).
Chama hicho ambacho kimekuwa madarakani tangu mwaka 1994, kimekuwa kikikabiliwa na tuhuma za mara kwa mara za rushwa na ubadhirifu wa fedha za umma, jambo ambalo limekuwa suala kuu la uchaguzi.