Maneno halisi ya makubaliano yaliyotiwa saini na viongozi wa Ethiopia na Somaliland hayajawekwa wazi, hilo linazusha tatizo kwani kuna kauli tofauti juu ya yale ambayo pande hizo mbili zilikubaliana katika Mkataba wa Makubaliano (MoU).
Wasomali wamepinga makubaliano ya bandari kati ya Ethiopia na Somaliland. Makubaliano hayo yamesababisha hasira nchini Somalia. Waziri wa ulinzi wa eneo lililojitangazia uhuru la Somaliland ameziujuzu kufuatia mzozo kuhusu makubaliano yenye utata ambayo yamesababisha mtafaruku katika Pembe ya Afrika. Abdiqani Mohamoud Ateye alijiuzulu akisema mawaziri wa baraza la mawaziri walipaswa kushauriwa kuhusu mpango ambao Somaliland ilitiliana saini na Ethiopia - wa kukodisha sehemu ya ufuo wake kwa nchi hiyo isiyo na bandari. Somalia - ambayo inaichukulia Somaliland kuwa sehemu ya ardhi yake - ilijibu kwa hasira makubaliano ya Januari 1, na kuyaita ''kitendo cha uchokozi.'' Marekani na Umoja wa Afrika zimeunga mkono Somalia katika mzozo huo na kuzitaka pande zote mbili kupunguza mivutano.
Maneno halisi ya makubaliano yaliyotiwa saini na viongozi wa Ethiopia na Somaliland hayajawekwa wazi, hilo linazusha tatizo kwani kuna kauli tofauti juu ya yale ambayo pande hizo mbili zilikubaliana katika Mkataba wa Makubaliano (MoU). MoU ni taarifa ya dhamira na si makubaliano ya kisheria lakini kinachoonekana ni kwamba Somaliland iko tayari kuipa Ethiopia eneo la bahari kwa shughuli za kibiashara kupitia bandari, ingawa haijulikani ni bandari gani. Pia kuna dhamira ya kijeshi. Somaliland imesema inaweza kukodisha sehemu ya pwani yake kwa jeshi la wanamaji la Ethiopia, jambo ambalo limethibitishwa na Addis Ababa. Kwa upande wake, Somaliland itapata mgao katika Shirika la Ndege la Ethiopia, shirika la taifa ambalo lina mafanikio makubwa. Lakini jambo lililoleta utata zaidi ni Ethiopia kusema itaitambua Somaliland kama taifa huru - jambo ambalo hakuna nchi nyingine imefanya au kuahidi katika kipindi cha miaka 30 tangu koloni la zamani Uingereza iondoke Somalia. Siku ya kutiwa saini, Rais wa Somaliland Muse Bihi Abdi alisema makubaliano hayo yanajumuisha Ethiopia kuitambua Somaliland kama nchi huru katika siku zijazo. Ethiopia haijathibitisha hilo. Badala yake, katika jaribio lake la kufafanua kilichopo kwenye makubaliano hayo; tarehe 3 Januari ilisema mpango huo ulijumuisha "tathmini ya kina kuhusu kuchukua msimamo juu ya juhudi za Somaliland kutambuliwa."
Kwa Somalia, Somaliland ni sehemu muhimu ya eneo lake. Hivyo kufanya makubaliano na nchi nyingine au sehemu ya eneo hilo kukodishwa bila idhini ya Mogadishu ni tatizo kubwa.
Siku moja baada ya MoU kutiwa saini, Somalia ilielezea mpango huo kama kitendo cha "uchokozi" ambacho ni "kizuizi cha amani na utulivu." Pia ilimwondoa balozi wake kutoka Addis Ababa.
Siku ya Jumapili, Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alikoleza msimamo kwa kusema: "Tutailinda nchi yetu, tutailinda kwa njia zote muhimu na kutafuta kuungwa mkono na mshirika yeyote aliye tayari kutusaidia."
Pia alitoa wito kwa vijana kujiandaa "kwa ajili ya ulinzi wa nchi yetu."
Wiki iliyopita kulikuwa na maandamano mjini Mogadishu kupinga mpango huo huku maelfu wakijitokeza kuelezea upinzani wao.
Somaliland, ilikuwa chini ya Uingereza, ilijitangazia uhuru kutoka Somalia mwaka 1991 na ina baadhi ya sifa za kuwa nchi, ikiwa ni pamoja na mfumo wa kisiasa unaofanya kazi, uchaguzi wa mara kwa mara, jeshi la polisi na sarafu yake yenyewe.
Kwa miongo kadhaa imeepuka machafuko na ghasia ambazo zimeikumba Somalia. Lakini uhuru wake haujatambuliwa na nchi yoyote.
Januari 3, Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Moussa Faki Mahamat alitoa wito wa utulivu na kuheshimiana na kuondoa mvutano unaoendelea kati ya Ethiopia na Somalia. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani, Matthew Miller pia alisema nchi yake ina wasiwasi na ripoti kwamba Ethiopia itatambua uhuru wa Somaliland. "Tunaungana na washirika wengine kuelezea wasiwasi wetu na kuongezeka kwa mvutano katika Pembe ya Afrika," alieleza katika mkutano na waandishi wa habari. Uturuki, ambayo ina ukaribu mkubwa na Somalia, ilisema "itajitolea kwa ajili ya umoja, mamlaka na uadilifu wa eneo la Somalia. Misri pia imeahidi kuiunga mkono Somalia. Rais Abdul Fattah al-Sisi alimwambia mwenzake wa Somalia, Misri inasimama upande wa Somalia na kuunga mkono "usalama na utulivu wake."