Simamieni fedha za miradi ya maendeleo kwa uadilifu’ mhe. nyamoga

Kamati ya kudumu ya Bunge ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa – TAMISEMI ikiongozwa na Makamu Mwenyekiti Mhe. Justine Nyamoga imewataka watumishi na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Urambo kusimiamia Miradi ya maendeleo kwa Uadilifu ili kuweza kufanikisha malengo na matakwa ya miradi ya mradi husika.


Mhe. Nyamoga ametoa rai hiyo katika kikoa cha majumuisho ya ziara ya ukaguzi ya utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya elimu kupitia program ya BOOST na SEQUIP ilijegwa katika Halmashauri hiyo Mkoani Tabora.

Amesema mifumo bora ya usimamizi mzuri ni mhimu katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo hivyo Serikali inapotoa Fedha za miradi Halmashauri inapaswa kuweka usimamizi bora na wa karibu ili fedha iliyotengwa iweze kufikia malengo maalumu ya miradi hiyo.


Aidha Mhe. Nyamoga amesema Kamati imeridhishwa na Utekelezaji na Maendeleo ya Miradi hii inayotekelezwa ambapo Mradi wa SEQUIP wa Shule ya Sekondari Igunguli iliyopo katika Kata ya Uyogo umetekelezwa na shule imeanza kutumika. 

Miradi hiyo ni pamoja na shule ya Sekondari Igunguli ambayo ina faida kubwa kwa wananchi wa kata ya Uyogo kwani hapo awali wanafunzi walilazimika kutembea umbali wa Kilomita 13 kwenda shuleni. 


Pia utekelezaji wa  Mradi wa BOOST wa shule ya Awali na Msingi Samia umetekelezwa katika Kata ya Urambo na shule ambapo tayari shule hiyo imeanza kutumika. Mradi wa shule hii umesaidia watoto wa kata ya Urambo kupata elimu kwenye mazingira ya karibu na makazi yao.

Akitoa neno la shukrani Mkuu wa Wilaya ya Urambo Dkt. Khamis Athumani Mkanachi ameishukuru kamati kwa kufanya ziara hiyo ya ukaguzi wa miradi katika Wilaya ya Urambo na kuahidi kutekeleza yale yote walioyaelekeza.

Share: