Shirika hilo linalenga kuendeleza haki na maadili ya demokrasia na linaendesha shughuli zake duniani kote.
Shirika la Ford Foundation lenye makao yake nchini Marekani limekanusha madai ya Rais William Ruto kwamba linafadhili maandamano ya kupinga serikali.
Katika taarifa walioitoa kwenye mtandao wao, Ford Foundation imesema, "Ingawa tunatambua haki ya Wakenya kutetea kwa amani nchi yenye haki na usawa, tunakanusha vitendo au matamshi yoyote ambayo yana chuki au kuunga mkono unyanyasaji dhidi ya taasisi yoyote, mtu binafsi au jamii yoyote. Hatukufadhili maandamano ya hivi majuzi dhidi ya mswada wa fedha na tuna sera isiyopendelea upande wowote kwa utoaji wetu wote wa ruzuku."
Haya yanajiri baada ya Rais William Ruto kulitaja shirika hilo na kulitaka kuambia Wakenya ukweli juu ya nani anayefadhili maandamano ya Kenya ya kupinga serikali.
Bw. Ruto aliongeza kuwa wote wanaohusika watakabiliwa na mkono wa sheria.
Shirika la Ford ni la kibinafsi lililoanzishwa mwaka 1963 na Edsel Ford, mtoto wa mwanzilishi wa Kampuni ya Ford Motor Henry Ford.
Shirika hilo linalenga kuendeleza haki na maadili ya demokrasia na linaendesha shughuli zake duniani kote.