Shilingi bil. 48 zimetengwa kwa wanafunzi wa stashahada-majaliwa

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika mwaka wa masomo 2023/2024 Serikali imetenga Sh. bilioni 48 kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wanafunzi wa ngazi ya stashahada.

Amesema hayo leo (Jumanne, Januari 16, 2024) wakati wa ufunguzi wa Chuo Kikuu Katoliki Mbeya (CUoM) mkoani Mbeya.

Amesema kuwa mpango huo ambao ni maono na maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan unalenga kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa bora na kuwezesha wahitimu wa vyuo nchini kujiamini na kumudu ushindani wa kitaifa na Kimataifa.

Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa Serikali imetenga Dola za Kimarekani milioni moja kupitia mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) ambazo zinasomesha Wahadhiri 27 kutoka Vyuo Vikuu visivyo vya Serikali.

 Waziri Mkuu ameongeza kuwa fedha hizo pia zitatumika katika kugharamia wahadhiri saba katika ngazi ya Shahada ya Umahiri na 20 katika Shahada ya Uzamivu kwa programu za afya na sayansi shirikishi.

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amesema Serikali inathamini na kutambua mchango wa madhehebu ya dini ikiwemo Kanisa Katoliki kwa kuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma kwenye sekta mbalimbali ikiwemo ya afya, elimu na ustawi wa jamii.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi la Baraza la Chuo hicho Askofu John Ndimbo ameishukuru Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) kwa kuona umuhimu wa kukipa chuo hicho hadhi ya chuo kikuu baada ya kutimiza masharti yote.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Franklin Rwezimula ambaye amemuwakilisha Waziri wa Elimu kwenye ufunguzi huo, amelipongeza Kanisa Katoliki kwa namna linavyowekeza kwenye sekta ya elimu.

Share: