Pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali, asasi za kiraia na jumuiya ya kimataifa, bado kuna changamoto nyingi katika kufikia usawa wa kijinsia.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema kazi kubwa imefanyika katika kipindi cha awamu hii ya uongozi kwa kutekeleza mikakati na sera zinazolenga kuondoa ubaguzi na kukuza usawa wa kijinsia.
Ametoa kauli hiyo (Jumapili, Desemba 3, 2023) wakati akizungumza na maelfu ya wananchi waliohudhuria kilele cha maadhimisho ya tatu ya kumbukumbu ya kumuenzi mwanasiasa mkongwe, Bibi Titi Mohammed yaliyofanyika kwenye viwanja vya Ujamaa, Ikwiriri, wilayani Rufiji, mkoani Pwani.
Waziri Mkuu ambaye alikuwa mgeni rasmi kwa niaba ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan alisema: “Pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali, asasi za kiraia na jumuiya ya kimataifa, bado kuna changamoto nyingi katika kufikia usawa wa kijinsia. Ukweli huo unatoa msukumo muhimu wa kuendeleza na kuimarisha juhudi zetu katika kushughulikia masuala ya usawa wa kijinsia,” amesema.
Akitaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa na Serikali ya awamu ya sita, Waziri Mkuu amesema ya kwanza ni kuongeza idadi ya wanawake katika nafasi za maamuzi ambapo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amekuwa akitoa fursa mbalimbali za uongozi kwa wanawake na kuimarisha uwiano katika teuzi anazozifanya kitendo ambacho kimeongeza idadi ya wanawake katika uongozi.