Serikali ya algeria imeahidi kuunga mkono msumbiji katika vita dhidi ya utekaji nyara na uasi

Serikali ya Algeria imeahidi kuunga mkono Msumbiji katika vita dhidi ya utekaji nyara na uasi wa kijihadi unaoathiri hasa jimbo la kaskazini la Cabo Delgado.

Makubaliano hayo yanakuja baada ya ziara ya siku nne ya Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi nchini Algeria.

Akiwahutubia waandishi wa habari siku ya Jumapili Rais Nyusi aliwaambia aliwaambia kwamba Algeria "imeahidi msaada wa haraka kwa Jeshi la Mitaa, ambalo linapambana na ugaidi".

Ameongeza kuwa, nchi hiyo ya Kaskazini mwa Afrika itatoa mafunzo kwa vikosi vyao na kutuma vifaa vya kuwasaidia katika mapambano yao dhidi ya makundi ya kijihadi.

Nchi hizo mbili zina uhusiano mkubwa wa kihistoria, kwani waasi wa kwanza wa vita vya ukombozi wa Msumbiji walipata mafunzo nchini Algeria.

Ahadi hiyo ya Algeria inakuja wakati ripoti kutoka Cabo Delgado zinasema wanajihadi waliopitia Quissanga Ijumaa usiku, waliiba chakula na kuzua hofu miongoni mwa wakazi.

Jimbo la Cabo Delgado lenye utajiri wa gesi limekuwa kivutio kwa makundi ya wanamgambo wenye itikadi kali yanayotaka kunyakuwa maliasili zake.

Makampuni mengi ya kimataifa yanafanya kazi katika eneo hilo.

Share: