Senegal: rais macky sall amesema ataondoka madarakani tarehe 2 aprili

Rais wa Senegal Macky Sall amesema ataondoka madarakani tarehe 2 Aprili wakati muhula wake utakapokamilika, lakini bado haijafahamika ni lini uchaguzi utafanyika ili kumchagua mrithi wake.

Alisema tarehe ya uchaguzi itategemea mdahalo wa kitaifa uliopangwa kuanza Jumatatu, ambao unajumuisha mashirika ya kiraia, vyama vya kisiasa na wagombea.

"Tarehe 2 Aprili 2024 dhamira yangu kama mkuu wa Senegal inafikia kikomo...ningependa mjadala huu utatuliwe kwa uwazi," alisema wakati wa mahojiano ya televisheni.

Tangazo lake linapunguza hofu kwamba alikuwa akipanga kuongeza muda wake, huku kukiwa na mzozo wa kisiasa.

Bw Sall amekuwa chini ya shinikizo la kutangaza tarehe ya uchaguzi tangu kujaribu kuuchelewesha mapema mwezi huu.

Alikuwa akitaka kuahirisha uchaguzi hadi Desemba ili mizozo kuhusu kustahiki kwa wagombea wengine iweze kutatuliwa.

Lakini mahakama kuu ya nchi hiyo ilisema kucheleweshwa huko ni kinyume cha katiba, na kutaka uchaguzi ufanyike "haraka iwezekanavyo".

Share: