Rea na tanesco msibebe changamoto za wakandarasi wabovu wachukulieni hatua

Naibu Waziri wa Nishati Mhe. Judith Kapinga amewataka Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kutobeba changamoto za wakandarasi wabovu na wanaolegalega katika kutekeleza Miradi ya Usambazaji wa Umeme Vijijini badala yake wawachukulie hatua kwa mujibu wa mikataba uliowekwa.

Mhe. Kapinga amesema hayo tarehe 6 Desemba, 2023 wakati wa ziara yake mkoani Tanga ya kukagua Maendeleo ya Miradi ya Usambazaji wa Umeme Vijijini katika Wilaya ya Korogwe, ambapo pamoja na mambo mengine ameeleza kuwa REA na TANESCO wakibeba changamoto hizo, inasababisha wananchi kufahamu kuwa wao ndiyo wenye matatizo.

Mhe. Kapinga amelazimika kusema hayo kufuatia kuwepo kwa mkandarasi wa Kampuni ya TONTAN kutounganisha umeme katika baadhi ya vijiji na vitongoji vya Wilaya ya Korogwe Vijijini kwa sababu mbalimbali.

Amesema Serikali imejitahidi sana kumsimamia huyo mkandarasi, imekaa naye mara nyingi ili kuona atamaliza lini kazi, lakini mkandarasi analegalega na siyo muungwana kwa sababu amepewa kazi ya kuunganisha watanzania ambao wanamahitaji ya umeme ili kuboresha hali zao za kiuchumi na bado ameendelea kulegalega hivyo hawatendei haki watu hao kwa sababu wanataka umeme ili waboreshe maisha yao.

"REA na TANESCO acheni kubeba changamoto za wa kandarasi wabovu na wanaolegalega kwa kuwa wananchi wanaona kuwa ninyi ndiyo wenye shida , msiwakingie vifua wala kuwatatulia changamoto zao hayo siyo matatizo yenu ni matatizo ya mkandarasi asiye muaminifu na hatutakubali mkandarasi mbovu aturudishe nyuma, TANESCO na REA kazi yenu ni kuwapa kazi wakandarasi na kazi hiyo inatakiwa kuisha desemba 2023 siku chache zimebaki kuanzia sasa", amesema Mhe. Kapinga.

Mkandarasi huyo alitakiwa kumaliza kazi desemba 30 mwaka huu, lakini mpaka sasa takribani siku 24 zimesalia mkandarasi huyo bado hajamaliza kazi, hivyo amewataka REA kutompa kazi tena Mkandarasi huyo hata kama atamaliza kazi hiyo kwa muda uliosalia na Serikali iko kazini kuhakikisha mkandarasi huyo anatekeleza kazi yake kwa mujibu wa mkataba.

Share: