Rc makonda kuanza ziara ya kikazi kwenye wilaya za mkoa wa arusha.

Kulingana na ratiba, Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema atafanya ziara yake Arusha Dc Mei 28, 2024

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda ametangaza kuanza kwa ziara ya Wilaya zote sita za Mkoa wa Arusha akisikiliza, kutatua kero za wananchi na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na serikali ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwenye uzinduzi wa magari ya uokoaji na zimamoto mkoa wa Arusha, Mhe. Makonda amesema katika ziara hiyo pia atakuwa na mikutano ya hadhara, akiwataka watendaji wa ngazi zote ngazi ya Mkoa kujiandaa ipasavyo kwani hatovumilia uzembe, ubadhirifu ama kusuasua kwa miradi ya maendeleo kunakofanywa kwa makusudi na baadhi ya watendaji.

Mhe. Mkuu wa mkoa amewaambia wananchi waliohudhuria uzinduzi huo wa magari ya Jeshi la zimamoto na uokoaji kuwa Mkoa wa Arusha unatakiwa kuwa namba moja katika usimamizi wa haki, kupiga vita vitendo vya rushwa na pia kuwa kinara katika uwajibikaji ili kuwa nguzo kuu ya watendaji wote wa mkoa wa Arusha.

Mkuu wa Mkoa Mhe. Paul Christian Makonda ametangaza kuwa ziara hiyo itaanza Alhamisi ya Mei 23 huko wilayani Longido kabla ya kuelekea Wilayani Karatu na baadae Mei 27 Mkuu wa Mkoa na ujumbe wake watakuwa wanaanza ziara wilayani Monduli.

Kulingana na ratiba, Mhe. Mkuu wa Mkoa amesema atafanya ziara yake  Arusha Dc Mei 28, 2024 na baadae kumalizia wilayani Meru Mei 29, 2024 na hitimisho la siku zake sita litakuwa kwenye eneo la Arusha Jiji tarehe 30, Mei 2024.

Mhe. Mkuu wa Mkoa ametoa rai kwa wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye mikutano yake ya hadhara na kuja kusema kuhusu haki zao zilizoporwa ama kuhusu watendaji wasiowajibika kikamilifu katika kumsaidia majukumu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Share: