Viongozi hao wa kiroho wametumia nafasi hiyo pia kumtaka Mhe. Makonda kutobadilika misimamo na tabia zake njema
Askofu Mkuu wa Kanisa la Waadventista Wasabato nchini Tanzania Dkt. Godwin Lekundayo na Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu la Kaskazini Mwa Tanzania Mch. Mark Malekana wamemuombea Kheri na Kumsihi Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Christian Makonda kuongeza jitihada katika kuwatumikia wananchi wa Arusha na kuwa sauti ya wananchi wanaokandamizwa na kuporwa haki zao.
Viongozi hao wa Kanisa la Waadventista Wasabato wamefika Ofisini kwa Mkuu wa Mkoa Mjini Arusha ili kumpongeza Mhe. Mkuu wa Mkoa kwa kuendelea kuaminiwa na Rais wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan pamoja na kumuombea kwa Mwenyenzi Mungu ili ampe nguvu zaidi, hekima na Utashi katika Majukumu yake ya sasa ya kuwatumikia wakazi wa Arusha.
Baba Askofu Mark Malekana katika maelezo yake amemtaja Mhe. Makonda kama kijana aliye mstari wa mbele katika kulipenda Taifa lake na kiongozi asiyekuwa na ubaguzi kutokana na kuunganisha makundi yote ya Kijamii hata yale yaliyokuwa yanaonekana kutokuwa na thamani kwenye jamii, akitolea mfano wa kundi la vijana wanaojiita 'Wadudu'.
Viongozi hao wa kiroho wametumia nafasi hiyo pia kumtaka Mhe. Makonda kutobadilika misimamo na tabia zake njema, na kusema kuwa Mungu anamtumia yeye ili kuwanufaisha anaowaongoza, wakimuomba Mungu pia aendelee kumpa nafasi zaidi za kiuongozi ili kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi.