Mh. Makonda ametaka Aprili 21, 2024 iwe mwisho kwa vitendo hivyo vya rushwa kwa Watendaji wa serikali ya Mkoa na kuahidi kushughulika kikamilifu na watendaji wanaokiuka
Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mh. Paul Christian Makonda amekemea vitendo vya rushwa na ubadhirifu kwa watumishi wa vitengo vya Ugavi na Manunuzi ndani ya Halmashauri ya mkoa wa Arusha, akisema anawafahamu watumishi wote wanaopokea rushwa kwenye utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Kikanuni Maafisa Ugavi na Manunuzi ndani ya Halmashauri zilizopo Nchini Tanzania wanawajibika kushughulikia manunuzi yote yanayofanywa na Halmashauri na kuandaa Nyaraka na Mikataba ya Zabuni pamoja na kuandaa matangazo ya zabuni mbalimbali.
Mh. Makonda ametaka Aprili 21, 2024 iwe mwisho kwa vitendo hivyo vya rushwa kwa Watendaji wa serikali ya Mkoa na kuahidi kushughulika kikamilifu na watendaji wanaokiuka miiko na maadili ya utumishi wa umma.
Mh.Mkuu wa Mkoa amefanya kikao kazi na watendaji na watumishi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Arusha ambapo pia amewataka kujitoa katika kuwatumikia wananchi badala ya kupambana kulinda nafasi zao bila ya kufanya kazi walizopewa katika kuwatumikia wananchi.
Mh. Mkuu wa Mkoa pia ameonya kuhusu Unafiki na Kujipendekeza kunakofanywa na watumishi na watendaji ndani ya mkoa wa Arusha na kuhimiza kazi ziwatambulishe zaidi kwa wananchi na Mamlaka zao za uteuzi.