Rc chalamila amezindua mfumo wa usajili wa vyeti vya watoto

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Mhe Albert Chalamila leo Novemba 28, 2023 amezindua mfumo wa usajili wa vyeti vya kuzaliwa vya watoto chini ya umri wa miaka mitano hafla ambayo imefanyika katika ukumbi wa Iddy Nyundo Manispaa ya Temeke Jijini Dar es Salaam.

RC Chalamila akiongea na Wataalam ambao walialikwa katika tukio hilo amesema Mkoa wa Dar es Salaam ni wa 26 kufikiwa na zoezi hilo tayari mikoa 25 imeshazindua mfumo huo wa usajili vyeti vya watoto.

Aidha Mhe RC Chalamila kwa kutambua unyeti wa Mkoa huo amewataka Viongozi katika maeneo mbalimbali wakiwemo wakuu wa Wilaya zote za Mkoa kusimamia zoezi hilo kwa weledi.

Vilevile ameelekeza Wakurugenzi kutoa usafiri katika utekelezaji za zoezi hilo ambapo ametoa shukrani kwa Kampuni ya Tigo, UNICEF na RITA kwa kuwezesha utekelezaji wa zoezi hili muhimu ambalo litaisaidia nchi kuwa na takwimu sahihi za watoto " Ni ukweli usiopingika cheti ni nyaraka muhimu kila mtu anatambua faida ya kuwa cheti cha kuzaliwa, na matumizi ya cheti hicho katika maisha ya kila siku niwaombe kuitumia fursa hiyo kikamilifu" Alisema RC Chalamila.

Mwisho Mkuu wa Wilaya ya Temeke Mhe Sixtus Mapunda amesema zoezi hilo kuzinduliwa Temeke ni sehemu sahihi kwa kuwa watoto ni wengi kuliko mahali pengine ambapo amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kusimamia zoezi hilo ipasavyo kwa masilahi mapana ya wanatemeke hivyo amemshukuru Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kuleta mfumo huo wa usajili wa vyeti vya kuzaliwa vya watoto nchi nzima.

Share: