Rais wa zamu wa eu viktor orban ataka kusitishwa kwa mapigano ya ukraine na urusi

Viktor Orban aliwasili Ukraine siku ya Jumanne kwa ziara ambayo haijatangazwa baada tu ya kuchukua nafasi ya rais wa zamu wa Umoja wa Ulaya.

Akiwa mjini Kyiv, waziri mkuu wa Hungary alisema kusitishwa kwa mapigano kati ya Urusi na Ukraine kunaweza kuharakisha mazungumzo ya kumaliza vita vilivyofuatia uvamizi wa Urusi mwaka 2022.

Bw Orban amekuwa mkosoaji wa uungaji mkono wa nchi za Magharibi kwa Ukraine na anaonekana kuwa kiongozi wa Ulaya aliye karibu zaidi na Rais wa Urusi Vladimir Putin. Hii ilikuwa ziara yake ya kwanza nchini Ukraine katika kipindi cha miaka 12, ingawa amekutana na Bw Putin mara kwa mara wakati huo.

Wakati wa kuonekana kwake pamoja na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky hakukuonekana kuwa na wasiwasi wowote kati yao lakini pia hakujibu maswali kutoka kwa vyombo vya habari baada ya kutoa taarifa zao.

Hapo awali Bw Orban alipunguza kasi ya makubaliano ya mfuko wa msaada wa Euro bilioni 50 ($54bn; £42bn) uliotengwa kusaidia Ukraine katika utetezi wake dhidi ya Urusi.

Lakini kwa muda wa miezi sita ijayo nafasi yake kama mkuu wa Baraza la Ulaya ina maana kwamba ana jukumu kubwa kama kiongozi wa Ulaya. Alikuja Ukraine katika siku yake ya pili katika jukumu hilo kwa majadiliano, akisema kuna haja ya kusuluhisha kutoelewana kwa hapo awali na kuzingatia siku zijazo.

Katika taarifa yake kufuatia mkutano wao, Bw Zelensky alisema ni "muhimu sana Ukraine kuungwa mkono na Ulaya kuendelea kudumishwa kwa kiwango cha kutosha... ni muhimu kwa ushirikiano kati ya majirani wote barani Ulaya kuwa wa maana zaidi na wa kunufaishana".

Katika taarifa yake mwenyewe, Bw Orban alisisitiza haja ya kufanya kazi pamoja lakini pia alisema ameibua wazo la kusitisha mapigano ili kuharakisha mazungumzo na Urusi.

Share: