Rais wa zamani wa ufilipino matatani kwa mauaji ya wauza madawa ya kulevya

Makamu wa Rais wa Ufilipino, Sara Duterte, amesema leo kuwa baba yake, ambaye ni rais wa zamani wa nchi hiyo, Rodrigo Duterte, atapelekwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu, ICC, mjini The Hague.

Amesema atasafirishwa kwa ndege kufuatia kukamatwa kwake leo asubuhi kwa mashitaka ya uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Katika taarifa yake, Sara amesema hatua iliyochukuliwa dhidi ya baba yake sio ya haki na ameitaja kuwa dhuluma na mateso.

Sara ameongeza kuwa baba yake ameshindwa kudai haki yake mbele ya mamlaka za mahakama nchini humo.

Mapema, Duterte alikuwa amesema kuwa anapaswa kufunguliwa mashtaka katika mahakama za Ufilipino na sio ile ya ICC.

Waranti wa ICC ulioonekana na shirika la habari la Reuters, unamshtumu Duterte kwa mauaji ya takribani watu 43 kati ya mwaka 2011-2019 kama sehemu ya vita vyake dhidi ya dawa za kulevya.

Share: