
Mahakama nchini Peru imemhukumu Rais wa zamani Alejandro Toledo kifungo cha miaka 13 na miezi 4 jela kwa kosa la utakatishaji fedha, ikiwa ni mara yake ya pili kutiwa hatiani kutokana na kashfa kubwa ya ufisadi.
Toledo, mwenye umri wa miaka 79, ambaye aliongoza Peru kati ya mwaka 2001 na 2006, alipatikana na hatia ya kutumia hongo kutoka kampuni ya ujenzi ya Brazil, Odebrecht (sasa ikijulikana kama Novonor), kununua mali ghali jijini Lima. Waendesha mashtaka walisema yeye na mkewe walitumia dola milioni 5.1 (sawa na shilingi bilioni 13.5 za Kitanzania) kununua nyumba na ofisi katika eneo la kifahari mjini Lima, pamoja na kulipia mikopo ya nyumba mbili nyingine. Fedha hizo zilipitishwa kupitia kampuni ya offshore nchini Costa Rica, iliyoundwa na Toledo kwa ajili ya kuficha asili ya fedha hizo.
Hukumu hii inakuja miezi kadhaa baada ya Oktoba 2024, ambapo Toledo alihukumiwa kifungo cha miaka 20 na miezi 6 kwa kupokea hongo ya hadi dola milioni 35 (sawa na shilingi bilioni 92 za Kitanzania) kutoka Odebrecht, ili kuipa kampuni hiyo zabuni kubwa za miradi ya miundombinu ya umma.
Katika kipindi chote cha kesi yake iliyodumu kwa mwaka mmoja, Toledo alikanusha mashtaka ya utakatishaji fedha na ushirikiano wa kifisadi yaliyowasilishwa dhidi yake. Mahakama imesema vifungo vyote viwili vitatekelezwa kwa pamoja.
Toledo, ambaye ni mchumi mwenye shahada kutoka Chuo Kikuu cha Stanford na Chuo Kikuu cha San Francisco, anatumikia kifungo chake katika gereza lililoko kwenye kambi ya polisi jijini Lima, ambalo maalum kwa viongozi wa zamani.
Wengine walioko katika kituo hicho maalum ni marais wa zamani Ollanta Humala na Pedro Castillo. Rais wa zamani Martin Vizcarra pia alikuwa akishikiliwa humo, lakini Jumatano hii mahakama kuu iliamuru aachiliwe kwa dhamana akisubiri kesi ya madai ya kupokea hongo zaidi ya miaka kumi iliyopita alipokuwa gavana wa Moquegua. Waendesha mashtaka wanapendekeza Vizcarra ahukumiwe miaka 15 jela, lakini amekanusha mashitaka akisema ni mateso ya kisiasa. Alitangaza pia nia ya kugombea urais tena mwaka 2026.
Kwa upande mwingine, rais wa zamani Pedro Pablo Kuczynski, mwenye umri wa miaka 86, bado anashtakiwa kwa kuhusishwa na sakata hilo, ambapo waendesha mashtaka wanataka apewe adhabu ya miaka 35 jela.
Kesi hizi zinahusiana na kashfa kubwa ya kimataifa ya ufisadi ya “Car Wash”, ambayo imeitikisa Amerika ya Kusini na kuwaangusha karibu marais wote wa Peru katika karne hii.