Rais wa urusi vladimir putin anatarajiwa kuizuru korea kaskazini kwa mara ya kwanza baada ya miaka 24

Marekani ilisema ina wasiwasi kuhusu "kuongezeka kwa uhusiano kati ya nchi hizi mbili"

Rais wa Urusi Vladimir Putin anatarajiwa kuizuru Korea Kaskazini kwa mara ya kwanza baada ya miaka 24 siku ya Jumanne.

Bw Putin atakutana na kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong Un kwa mazungumzo katika mji mkuu Pyongyang.

Viongozi hao wawili walikutana mara ya mwisho mwezi Septemba katika mji wa Vladivostok nchini Urusi lakini hii ni mara ya kwanza kwa Putin kutembelea Pyongyang tangu 2000.


Marekani ilisema ina wasiwasi kuhusu "kuongezeka kwa uhusiano kati ya nchi hizi mbili".

Ikulu ya Kremlin imeelezea tukio hilo kama "ziara ya kirafiki ya serikali" huku vyombo vya habari vya Urusi vikiripoti kuwa Bw Putin na Bw Kim wanaweza kutia saini makubaliano ya ushirikiano, ikiwa ni pamoja na masuala ya usalama, na watatoa taarifa za pamoja kwa vyombo vya habari.

Gwaride katika mraba wa Kim Il Sung linatarajiwa. Bw Putin pia anatarajiwa kushuhudia tamasha na kuzuru Kanisa la Kiorthodox la Life-Giving Trinity huko Pyongyang, kanisa pekee la Kiorthodox nchini Korea Kaskazini.

Kuna ripoti kwamba Bw Putin atakaa katika nyumba ya wageni ya Kumsusan huko Pyongyang, ambapo kiongozi wa China Xi Jinping alikaa mara ya mwisho wakati wa ziara yake ya kitaifa nchini Korea Kaskazini mnamo 2019.

Bw Putin anatarajiwa kuwasili na waziri wake mpya wa ulinzi, Andrei Belousov, huku Waziri wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov, na Naibu Waziri Mkuu Alexander Novak pia wakiwa katika ujumbe huo.

Rais wa Urusi aliipongeza Korea Kaskazini kwa "kuunga mkono kwa uthabiti" vita vya Urusidhidi ya Ukraine kabla ya ziara yake.

Share: