Kama mshirika asiye wa Nato, Kenya itakuwa na fursa ya kupata vifaa vya kisasa vya kijeshi, mafunzo na mikopo.
Hii ina maana kwamba licha ya Kenya kutokuwa katika sehemu ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO, ina ushirikiano wa kina wa kimkakati na usalama na Marekani.
Uteuzi huo unajiri wiki chache baada ya ziara ya kitaifa ya Rais William Ruto nchini Marekani.
"Kwa mamlaka niliyopewa kama Rais na Katiba na sheria za Marekani, ikiwa ni pamoja na kifungu cha 517 cha Sheria ya Usaidizi wa Kigeni ya 1961, kama ilivyorekebishwa nateua Kenya kama Mshirika Mkuu asiye wa NATO wa Marekani kwa madhumuni ya Sheria ya Kudhibiti Usafirishaji wa Silaha ‘’, ulisema uamuzi wa rais wa Marekani wa tarehe 24 Juni.
Ni wakati wa ziara ya rais Ruto nchini Marekani ambapo Biden alitangaza nia yake ya kuwa na Kenya kama mshirika mkuu asiye wa NATO.
NATO ambayo inawakilisha Shirika la Mkataba wa Atlantiki ya Kaskazini kwa sasa ina nchi wanachama 32, zinazoitwa washirika wa NATO.
Hatua hii ya kihistoria ya Biden inaashiria hatua muhimu kwa Kenya kwani inakuwa taifa la kwanza la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara kupokea hadhi hii na la nne barani Afrika.
Mataifa mengine yaliotunukiwa hadhi hii ni pamoja na Misri iliyotunukiwa na Rais wa zamani Ronald Reagan (1987), Morocco na George W. Bush (2004), na Tunisia na Barack Obama mwaka 2015. Ikulu ya White House ilisema hadhi hii ya kifahari imetolewa na Marekani kwa nchi ambazo zinadumisha uhusiano wa karibu na wa kimkakati wa kijeshi na ulinzi.
"Marekani inaheshimu sana mchango mkubwa wa Kenya kwa amani na usalama duniani," ilisema.
Kwa miongo kadhaa, ushirikiano thabiti wa usalama kati ya mataifa hayo mawili umekuwa na jukumu muhimu katika kudumisha utulivu katika Afrika Mashariki na kwingineko.
Kama mshirika asiye wa Nato, Kenya itakuwa na fursa ya kupata vifaa vya kisasa vya kijeshi, mafunzo na mikopo.
Hata hivyo, Marekani haina wajibu wa kuipatia msaada wa kijeshi wa moja kwa moja na Kenya haina mamlaka ya kutuma wanajeshi kwa ajili ya operesheni za Nato.
Nchi zilizo chini ya hali hii hupokea manufaa mbalimbali ya kijeshi na kifedha lakini hazina ahadi za ulinzi wa pande zote ambazo wanachama wa NATO wanazo chini ya Kifungu cha 5 cha mkataba wa NATO.