Mawakili wa familia hiyo wanasema pia wamewasilisha malalamiko katika mahakama ya Paris
Rais wa Gabon aliyeondolewa madarakani, Ali Bongo na wanawe wawili wamegoma kula chakula kwa kulalamikia madai ya kujitiisha kwa "vitendo vya mateso na ukatili", mawakili wa familia hiyo wanasema.
Bw Bongo alitimuliwa katika mapinduzi ya kijeshi mwezi Agosti mwaka jana, muda mfupi baada ya kushinda kura ya urais iliyozozaniwa.
Kisha alizuiliwa nyumbani kwake katika mji mkuu, Libreville, pamoja na wanawe wawili, Jalil na Bilal.
Junta pia iliwashikilia mkewe Sylvia Bongo na mwanawe mkubwa Noureddin gerezani, wakisubiri kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za rushwa.
Katika taarifa, mawakili wao walidai kuwa Noureddin na Sylvia walipigwa na kunyongwa wakiwa kizuizini.
Pia wanadai kuwa Noureddin aliteswa, kuchapwa viboko na "hata kupigwa na umeme kwa taser".
Rais huyo aliyeondolewa madarakani, mwenye umri wa miaka 64, aliongoza nchi hiyo yenye utajiri mkubwa wa mafuta tangu 2009 alipomrithi baba yake ambaye amekuwa madarakani kwa zaidi ya miaka 40.
Mawakili wa familia hiyo wanasema pia wamewasilisha malalamiko katika mahakama ya Paris, wiki moja kabla ya kiongozi wa serikali ya Gabon Brice Oligui Nguema kuzuru Ufaransa.