Akiwa tayari ofisini kwa takriban robo karne na kiongozi wa Kremlin aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi tangu Josef Stalin
Vladimir Putin alianza muhula wake wa tano kama Rais wa Russia katika sherehe za kuapishwa zilizofanyika Kremlin, akianza miaka mingine sita madarakani baada ya kuwaangamiza wapinzani wake wa kisiasa, kuanzisha vita vikali nchini Ukraine na kulidhibiti taifa hilo.
Akiwa tayari ofisini kwa takriban robo karne na kiongozi wa Kremlin aliyehudumu kwa muda mrefu zaidi tangu Josef Stalin, muhula mpya wa Putin utakamilika 2030, wakati atakapokuwa na nafasi nyingine ya kugombea kikatiba.
Katika hafla hiyo ndani ya Jumba la Grand Kremlin, Putin aliweka mkono wake kwenye Katiba ya Russia na kuapa kuitetea huku umati wa watu mashuhuri walioalikwa wakitazama.
Tangu kumrithi Rais Boris Yeltsin 1999, Putin ameibadilisha Russia kutoka nchi iliyoibuka kutoka kwa mporomoko wa kiuchumi hadi inayoonekana kutishia usalama wa ulimwengu. Kufuatia uvamizi wa Ukraine wa 2022 ambao umekuwa mzozo mkubwa zaidi barani Ulaya tangu Vita vya Kidunia vya pili, Russia imewekewa vikwazo vikali na nchi za Magharibi na inageukia serikali nyingine kama China, Iran na Korea Kaskazini kwa msaada.