Kiswahili ni lugha ya ukombozi, ni lugha ya umoja, ni lugha ya amani na ni lugha ya biashara
Rais wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesema Kiswahili ni lugha ya ukombozi, umoja, amani na pia lugha ya biashara huku akiwataka Viongozi na Wananchi kote Ulimwenguni kutumia Kiswahili katika kulinda amani na kukuza biashara.
Rais Samia amesema hayo katika ujumbe alioutoa July 07,2024 katika Maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani ambapo amesema “Ni fahari kwa Tanzania kuwa sehemu ya maadhimisho ya lugha ya Kiswahili yenye Wazungumzaji takribani milioni 200 ndani na nje ya Afrika, Kiswahili kimesambaa kwa mapana na marefu kutoka Japan hadi Marekani, kutoka Finland hadi Afrika Kusini, Kiswahili ni lugha tunayojivunia”
“Kutangazwa July 07 kama siku maalum ya Kiswahili ni miongoni mwa matunda ya jitihada, nafarijika kwamba juzi July 01,2024 Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwa kauli moja lilipitisha kuitambua July 07 kuwa siku ya Kiswahili”
“Kiswahili ni lugha ya ukombozi, ni lugha ya umoja, ni lugha ya amani na ni lugha ya biashara, nitoe rai kwa Viongozi wenzangu kote Ulimwenguni kukitumia Kiswahili katika kukuza mtengamano, kujenga na kulinda amani na mshikamano, kufundisha Watoto na Vijana wetu elimu na maadili mema na kukuza biashara miongoni mwa Nchi zetu”