Rais samia suluhu hassan ametoa fedha kwaajili ya ujenzi wa kituo kikubwa cha mabasi cha mkoa wa arusha

Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini Mhe. Mrisho Mashaka Gambo amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha kwaajili ya Ujenzi wa kituo kikubwa cha Mabasi cha Mkoa wa Arusha, kituo kinachotarajiwa kuanza kujengwa hivi karibuni.

Mhe. Gambo ametoa kauli hiyo leo Aprili 27, 2024 wakati wa Mkutano mkuu wa Jimbo alipokuwa akieleza kuhusu utekelezaji wa ilani ya Chama Cha Mapinduzi kwenye Jimbo la Arusha Mjini.

Mhe. Gambo amewaambiwa wananchi na Wajumbe wa Mkutano huo kuwa tayari ekari 30 zimepatikana kwaajili ya ujenzi wa Kituo cha Mkoa cha Mabasi eneo la Bondeni City Kwenye Kata ya Murieti Pembezoni kidogo mwa Jiji la Arusha.

Katika Hatua nyingine pia Gambo ameishukuru serikali kwa ujenzi na ukarabati wa Barabara za ndani ya Jimbo lake, zaidi ikiwa ni barabara ya Njia nne itakayojengwa kutokea Uwanja wa Ndege Kisongo mpaka soko la Kilombero.

Mhe. Gambo amesema ujenzi wa barabara hiyo ni muendelezo wa Ujenzi wa Miundombinu ndani ya Mkoa huo ikiwa ni maandalizi ya uenyeji wa michuano ya kandanda barani Afrika maarufu kama Afcon, inayotarajiwa kuchezwa mwaka 2027, wenyeji wakiwa ni Tanzania, Kenya na Uganda.

Mbunge huyo pia amewaambia wana Arusha kuwa tayari serikali imetenga fedha kwaajili ya Ujenzi wa masoko makubwa na ya kisasa ya Kilombero na Kwa Mrombo na mchakato wa ujenzi wake unaendelea.

Kwa upande wa Elimu Mhe. Gambo ametaja shule mpya zilizojengwa kwenye miaka mitatu ya Rais Samia Suluhu Hassan ikiwemo shule za msingi Maasai, NAFCO Olmoti na Msasani B Murriet.

Kwa Upande wa shule za sekondari Shule zilizojengwa na serikali ya Rais Samia ni pamoja na shule ya Sekei, Kalimaji Moshono na shule ya sekondari Unga Limited.

Kwa Upande wa sekta ya Afya hususani kwenye Hospitali ya Mkoa Mount Meru, Mhe. Gambo amesema hospitali hiyo imepatiwa mashine ya CT-Scan, Mashine mpya ya Xray pamoja na ongezeko kubwa la bajeti za dawa mbalimbali.

Katika hatua nyingine Mhe. Gambo ameshukuru ushirikiano mkubwa alioupata kutoka kwa viongozi wenzake ndani ya Mkoa na kuahidi kuandaa mikutano ya hadhara hivi karibuni ili kuwaeleza wananchi utekelezaji wa ahadi na ilani ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2023/24.

Katika Mkutano huo wananchi walichangisha fedha kwaajili ya kumchukulia fomu ya kugombea Urais, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan atakayekuwa anatetea kiti chake katika uchaguzi mkuu wa 2025.

Share: