Rais paul kagame ameahidi kuilinda nchi yake dhidi ya uchokozi wa nchi jirani

Rais wa Rwanda Paul Kagame ameahidi kuilinda nchi yake dhidi ya uchokozi wa nje wakati mvutano ukiongezeka kati ya Kigali na nchi jirani za Burundi na DR Congo.

"Linapokuja suala la kuitetea nchi hii ambayo imeteseka kwa muda mrefu na hakuna aliyekuja kusaidia, hatuhitaji ruhusa kutoka kwa mtu yeyote kufanya kile tunachotakiwa kufanya ili kujilinda," alisema Kagame katika hotuba iliyorushwa na televisheni ya taifa ya Rwanda jana.

Akiwahutubia wajumbe katika mkutano wa majadiliano ya kitaifa, Kagame kwa mara nyingine alikanusha madai ya DRC kwamba Rwanda inawaunga mkono waasi katika maeneo ya mashariki mwa Congo.

Akizungumzia mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 dhidi ya Watutsi, rais alisema: "Kama kuna atakayetufanya tunafikirie kama tunarudi nyuma katika nyakati hizo, basi hatuna cha kupoteza. Tutapigana kama watu ambao hawana kitu cha kupoteza."

Rwanda imeingia katika mzozo wa kidiplomasia na Burundi, ambayo ilifunga mpaka wa pamoja tarehe 11 Januari baada ya kuihusisha Rwanda na shambulio la kigaidi lililofanywa na waasi wa RED-Tabara mwezi Disemba.

Jana, Burundi ilikanusha madai ya Rwanda kwamba Rais Evariste Ndayishimiye alitoa wito wa kuondolewa mamlakani kwa Kagame wakati wa hotuba yake aliyoitoa katika Jamuhuri ya kidemokrasi ya Congo Januari 21.

Share: