Rais dkt. william ruto yuko tayari kufanya mazungumzo na maelfu ya vijana waliofanya maandamano nchini kenya

Kwa mara ya kwanza tangu kuanza kwa maandamano ya kupinga mapendekezo ya nyongeza ya kodi Nchini Kenya, Rais wa Nchi hiyo Dkt. William Ruto ametoa tamko lake la kwanza hadharani ambapo amesema yuko tayari kufanya mazungumzo na maelfu ya Vijana waliofanya maandamano ya amani wiki hii kote Nchini huku akiwapongeza Vijana hao kwa kujitokeza na kushughulika na mambo ya Taifa lao.

Maandamano hayo yaliandaliwa kwenye mitandao ya kijamii kisha yakahamia kwenye barabara mbalimbali za Kenya huku Washiriki wakubwa wakiwa ni Vijana Wakenya wengi wenye umri mdogo maarufu kama ‘Gen-Z’ ambao wamekuwa wakipeperusha maandamano hayo moja kwa moja kwenye mitandao ya kijami wakishinikiza kutoridhika kwao kuhusu sera za kiuchumi za Serikali ya Rais RUTO.

Akizungumza akiwa kwenye Kanisa moja katika Mji wa Nyahururu katika eneo la Bonde la Ufa, Dkt. Ruto amesema “Ninajivunia sana Vijana wetu, wamepiga hatua mbele kwa kufanya maandamano ya amani na ninataka kuwaambia kwamba tutawashirikisha Ruto amesema Serikali yake itafanya mazungumzo na Vijana hao ili kwa pamoja walijenge Taifa la Kenya liwe kubwa zaidi.”

Share: