Prof.nagu aongoza kikao cha wizara ya afya na wadau cha mpango jumuishi na endelevu wa kuratibu wahudumu wa afya ngazi ya jamii.

Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Tumaini Nagu Novemba 7, 2023 ameongoza kikao baina ya Wizara ya Afya na wadau cha kutoa maoni kuhusu Mpango Jumuishi na Endelevu wa kuratibu Wahudumu wa Afya Ngazj ya Jamii (Stakeholders Meeting on Integrated and Coordinated Community Healthy Workers Program).

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika Jijini Dar Es Salaam Mganga Mkuu wa Serikali Prof. Nagu amesema Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wana umuhimu mkubwa katika utoaji wa huduma za afya ngazi ya jamii hivyo kupitia kikao hicho cha kupitia Mpango huo itakuwa na chachu kubwa katika uimarishaji wa huduma za afya ngazi ya jamii.

“Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wana umuhimu kwani wao ndio wanaosaidia kutoa elimu ya afya ngazi ya chini kabisa ya kijiji hivyo kupitia Mpango Jumuishi itakuwa chachu kubwa katika utoaji wa huduma za afya ngazi ya jamii mfano elimu juu ya lishe, utapiamlo” amesema.

Nae Mkurugenzi wa Idara ya Kinga kutoka Wizara ya Afya Dkt. Ntuli Kapologwe amesema Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii wana mchango mkubwa katika kusambaza ujumbe kuhusu masuala mbalimbali ya afya hasa katika eneo la kinga dhidi ya magonjwa ngazi ya jamii, huku Mkurugenzi wa Huduma za Tiba Prof. Pascal Ruggajo akisema kupitia Programu hiyo inasaidia katika kuhakikisha suala la tiba halina kikwazo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Elimu ya Afya kwa Umma kutoka Wizara ya Afya Dkt.Tumaini Haonga ameainisha baadhi ya mikakati kabambe inayotumika katika uimarishaji wa huduma za afya ngazi ya jamii kuwa ni pamoja na kutoa elimu ya afya katika mapambano ya magonjwa mbalimbali ikiwemo Virusi vya UKIMWI na UKIMWI, Malaria, Kifua Kikuu (TB), magonjwa ya mlipuko kama Kuhara ikiwemo Kipindupindu.

Ikumbukwe kuwa kuanzishwa kwa Mpango Jumuishi na Endelevu wa Kuwatumia Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii una lengo la kuharakisha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote hususan katika ngazi ya msingi ambapo inalenga kuvifikia vijiji 12,318, mitaa 4,263 na vitongoji 64,384 nchi nzima.

Share: