Polisi nchini kenya imepiga marufuku maandamano katika ya jiji la nairobi

Raia waliombwa kuwa makini katika maeneo yenye watu wengi, kushirikiana na polisi na kutoa taarifa

Idara ya Huduma ya Polisi nchini Kenya imepiga marufuku maandamano katika ya jiji la Nairobi na viunga vyake na kutoa hakikisho la usalama katika eneo hilo.

Katika taarifa yake iliyotolea Julai, 17, 2024, imekumbusha umma jukumu muhimu la idara hiyo katika usalama wa nchi kulingana na katiba.

Hayo yamejiri huku Kenya ikiendelea kushuhudia maandamano ambayo yalianza tangu mwezi Juni, kupinga Mswada wa Fedha 2024.

‘’Nchi yetu imekuwa ikishuhudia hasara kubwa, watu wamejeruhiwa, kupoteza maisha, mali na biashara zimeharibiwa,’’ taarifa ya Idara ya Huduma ya Polisi ilisema.

Iliendelea kusema kuwa imepokea taarifa kwamba baadhi ya makundi ya kihalifu yanapanga kutumia vibaya maandamano ya siku ya Alhamisi, Julai 18, 2024 kutekeleza mashambulizi na uhalifu.

Idara hiyo ilielezea ukosefu wa uongozi kuwa imefanya kuwa vigumu kufanyika kwa maandamano ya amani katika siku zilizopita.

"Kukosekana kwa uongozi katika maandamano yaliyopita kumefanya kuwa vigumu kuhakikisha itifaki za usalama zinafuatwa. Kwa sababu hiyo, hakuna maandamano yataruhusiwa katika eneo la kibiashara katikati ya mji wa Nairobi na viunga vyake kwenda mbele kuhakikisha usalama wa raia," polisi ilisema.

Raia waliombwa kuwa makini katika maeneo yenye watu wengi, kushirikiana na polisi na kutoa taarifa zozote ambazo zinaweza kusaidia kubaini uhalifu.

Share: