Waasi wa Houthi wanasema mashambulizi yao ni ishara ya kuwaunga mkono Wapalestina katika vita kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza.
Nyaya kadhaa za mawasiliano chini ya bahari katika Bahari ya Shamu zimekatwa, na kuathiri 25% ya trafiki ya data kati ya Asia na Ulaya, kampuni ya mawasiliano ya simu na afisa wa Marekani wanasema.
Kampuni ya HGC Global Communications yenye makao yake Hong Kong ilisema kuwa imechukua hatua za kubadilisha trafiki baada ya kebo nne kati ya 15 kukatwa hivi majuzi.
Sababu bado haijawekwa wazi. Afisa huyo wa Marekani alisema ilikuwa ikijaribu kubaini iwapo nyaya hizo zilikatwa kimakusudi au kung'olewa na nanga.
Mwezi uliopita, serikali ya Yemen inayotambuliwa kimataifa ilionya kwamba waasi wa kihouthi wanaoungwa mkono na Iran huenda wakaharibu nyaya za chini ya bahari pamoja na kushambulia meli baharini.
Wahouthi - ambao wanadhibiti sehemu kubwa ya pwani ya Bahari ya Shamu magharibi mwa Yemen - wiki iliyopita walikanusha kuhusika na uharibifu wa nyaya hizo na kuelekeza kidole cha lawama kwa mashambulizi ya kijeshi ya Marekani na Uingereza.
Vikosi vya Marekani na Uingereza vimelenga silaha na miundombinu ya Houthi katika kukabiliana na mashambulizi ya ndege zisizo na rubani na makombora dhidi ya meli za wafanyabiashara zinazopitia Bahari ya Shamu na Ghuba ya Aden.
Waasi wa Houthi wanasema mashambulizi yao ni ishara ya kuwaunga mkono Wapalestina katika vita kati ya Israel na Hamas katika Ukanda wa Gaza.