
Burkina Faso, Mali na Niger zimetangaza uamuzi wao wa kujiondoa mara moja kuwa wanachama wa mahakama ya kimataifa inayoshughulikia kesi za uhalifu wa kivita na kibinadamu ICC,zikidai mahakama hiyo ni chombo cha kuendekeza ukoloni mambo leo na ubaguzi katika hukumu zake.
Mataifa hayo matatu ya ukanda wa Sahel katika taarifa ya pamoja iliyoidhinishwa na Jenerali Assimi Goita rais wa Mali imeshutumu ICC kwa kuwaandama bila kukoma viongozi fulani hasa wa kutoka mataifa masikini na kudhihirisha kushindwa kuwahukumu wanaofanya uhalifu mbaya zaidi ulimwenguni.
Uamuzi huo ndiyo wa hivi karibuni kutoka kwa mataifa hayo matatu ya magharibi mwa Afrika ynayoongozwa kijeshi ambayo pia mwaka huu yalijiondoa kutoka jumuiya ya maendeleo ya nchi za magharibi mwa Afrika ECOWAS na kuanzisha jumuiya ya mataifa ya Sahel AES.
ICC iliyoanzishwa mwaka 2002 ilitiwshwa jukumu la kushughulikia kesi za mauaji ya halaiki,uhalifu dhidi ya binadamu na vita na tangu wakati huo imepokea mashitaka thelathini na tatu.
Wakosoaji wa ICC wanasema mahakama hyiyo inawalenga viongozi wa Afrika lakini wanaoiunga mkono wanahoji mfumo dhaifu wa idara za mahakama katika mataifa ya Afrika zinalazimu asasi na watu binafsi kutafuta haki katika mahakama hiyo ya kimataifa.