Nato yaadhimisha miaka 70 ya kuanzishwa kwake

Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg ameihimiza Marekani kuendelea kuwa pamoja na Ulaya, wakati Jumuiya hiyo ya kijeshi ya nchi za Magharibi ikiadhimisha miaka 75 tangu kuundwa kwake huku ikikabiliwa na changamoto kubwa.

Akizungumza katika hotuba ya kuadhimisha miaka 75 tangu kuasisiwa kwa Jumuiya hiyo ya kujihami NATO, Jens Stoltenberg amesema Ulaya na Marekani zinahitajiana kwaajili ya usalama wao. Amesema Ulaya inaihitaji Marekani na Marekani ya kaskazini inaihitaji Ulaya kwa usalama huo. Stoltenberg amesema washirika wa Ulaya wanatoa kiwango cha juu kabisa cha jeshi, mitandao mipana ya kijasusi na fursa ya kidiplomasia. Amesema kupitia NATO Marekani ina marafiki na washirika wengi zaidi kuliko taifa lolote lililo na nguvu duniani.

Wakati Jumuiya hiyo ikiadhimisha miaka hiyo 75 ya uwepo wake, nchi wanachama 32 wa Jumuiya hiyo walikubaliana kuanza kupanga jukumu kubwa katika kuratibu msaada wa kijeshi kwa Ukraine, kuisaidia kupambana na uvamizi wa Urusi ulioanza mwezi Februari mwaka 2022, uvamizi uliosababisha mgogoro mkubwa zaidi kuwahi kuonekana barani Ulaya, tangu kumalizika kwa vita vya pili vya dunia.

Stoltenberg aliwataka wanachama kuonyesha umoja wao kwa Ukraine wakati taifa hilo la zamani la Kisovieti likisubiri msaada wa dola bilioni 60 ambao umeshindwa kupitishwa na bunge la Marekani.

Viongozi wa Ulaya walio wengi katika Jumuiya ya NATO wana wasiwasi sio tu kuhusu siku za usoni za Jumuiya hiyo iwapo rais wa zamani wa Marekani Donald Trump atamshinda mpinzani wake rais wa sasa wa Marekani Joe Biden katika uchaguzi wa Novemba mwaka huu, lakini pia juu ya msaada wa fedha kwa Ukraine uliokwama kuidhinishwa Marekani kufuatia wanachama wa Republican kutaka hakikisho pana la usalama kabla ya kupitisha muswada huo.

Share: