Mwili wa Gardner g. habash kupumzishwa leo kikelelwa kata ya tarakea wilayani rombo

Udongo wa Kikelelwa Kata ya Tarakea Wilayani Rombo, Kilimanjaro unajiandaa kumpokea na kumpumzisha aliyekuwa Mtangazaji kinara wa Clouds Media Group kwa zaidi ya miaka kumi sasa Bwana Gardner G. Habash.

Zawadi kubwa nyingi ametuachia, moja ikiwa ni darasa alilotupatia kwa vitendo juu ya namna ya kuishi vyema na watu pamoja na ubunifu wake mkubwa katika kutangaza na kutengeneza matangazo mbalimbali ya Sauti. Ameishi nasi miaka 51, miaka iliyojaa mafunzo mengi ambayo kila mmoja anaweza kujifunza kutoka kwake kwa namna tofauti.

Simulizi na hadithi nzuri zimetapakaa kona zote za nchi na kwenye Vyombo mbalimbali vya habari - Maudhui ni yaleyale, Gardner aliishi vyema na watu na hata watangazaji wenzake wanamtaja kama Kaka wa mfano "Role Model" kutokana na alivyoishi na wengine kwenye vyumba vya habari na hata kwa ndugu, jamaa na marafiki.

Safari yake ya Mwisho inaanza leo. Zile Nakshi na sauti tuliyokuwa tumeizoea masikioni mwetu mara zote tuwashapo Redio zinafikia mwisho wake rasmi hii leo hapa kijijini Kikelelwa.


Mwili wa Gardner G.Habash Mtangazaji wa Kituo cha Clouds Media Group na Mshereheshaji wa matukio mbalimbali utapumzishwa hapa kwenye Makaburi ya Familia kijijini Kikelelwa, Kata ya Tarakea Mkoani Kilimanjaro.

Wengi tulimuita Kaka kwenye Tasnia hii ya Habari kutokana na ubunifu wake na kipaji cha hali ya juu kilichokuwa kikinakshiwa na Sauti nzito ya mirindimo ya kupanda na kushuka na leo Udongo wa Rombo unakwenda kufukia mambo yote hayo yaliyokuwa ndani yake akituachia mafunzo mengi mazuri kutoka kwenye Maisha yake binafsi na Maisha ya kazi.

Gardner G. Habash anazikwa pembezoni kabisa na alipozikwa Mama yake mzazi Clementina Habash ambaye alipumzishwa hapa Julai Mwaka 2021.

Share: