Mwigulu na aweso washuhudia kusainiwa mkataba wa mradi wa usambazaji maji ya ziwa victoria kutoka kahama hadi ushetu wa zaidi ya bilioni 44

miradi itakayohusika katika programu hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa kilomita 76 za bomba kuu kutoka Manispaa ya Kahama kwenda hadi Ulowa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuongeza Bajeti ya Wizara ya Maji ili kuimarisha sekta ya maji nchini kote na kumtua mama ndoo kichwani.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati akihutubia maelfu ya wananchi wa Jimbo la Ushetu, katika Hafla ya utiaji saini kandarasi ya ujenzi wa mradi wa usambazaji maji ya Ziwa Victoria kutoka Manispaa ya Kahama kwenda Halmashauri ya Ushetu ambayo Imefanyika leo tarehe 2 Juni, 2024 katika Viwanja vya Shule ya Msingi Kangeme, iliyopo Kata ya Ulowa, Halmashauri ya Ushetu mkoa wa Shinyanga.

Akiongea na hadhara hiyo , Dkt. Nchemba alisema kuwa Mradi huo wa maji ya Ziwa Victoria katika Halmashauri ya Ushetu utachochea maendeleo ya Halmashauri hiyo kwa kutoa fursa mbalimbali kwa Wananchi ikiwemo kupata muda mwingi wa kufanya shughuli za kiuchumi kama vile kilimo cha umwagiliaji na ufugaji. 

Aidha, Dkt. Nchemba alisema kuwa mradi huo utasaidia kuimarisha Afya za Wananchi kwa kupunguza magonjwa yatokanayo na matumizi ya maji yasiyo safi na salama kama vile kipindupindu. 

Naye Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso (Mb), akizungumza na wananchi, alisema kuwa katika kuhakikisha Serikali inamtua mama ndoo kichwani na kutambua adhima ya Serikali chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini kwa kushirikiana na Mamlaka za Maji (KASHWASA, KUWASA na SHUWASA) imekamilisha usanifu wa mradi huo, ambapo ujenzi wake utahusisha ujenzi wa miundombinu ya majisafi na salama.

Mhe. Aweso alisema kuwa taratibu za kupata Mkandarasi kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi zimefanyika na kukamilika na sasa utekelezaji wa mradi utaanza baada ya tukio la kusainiwa kwa Mkataba na utekelezaji wake utafanywa na Kampuni ya Sihotech Engineering Company Limited kwa gharama ya shilingi bilioni 44.

Aliitaja miradi itakayohusika katika programu hiyo kuwa ni pamoja na ujenzi wa kilomita 76 za bomba kuu kutoka Manispaa ya Kahama kwenda hadi Ulowa kwenye matanki ya maji lenye kipenyo cha ukubwa wa kuanzia mm.350 hadi mm.100, Ujenzi wa kilomita 74 za mabomba kwenye mtandao wa kusambaza maji yenye ukubwa wa mm. 160, 110, 90, 75, 63, 50, 40, na 32, Ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji la lita 500,000 katika eneo la Ulowa Na.2, Ujenzi wa tanki la kuhifadhia maji la lita 300,000 katika eneo la Ulowa Na.4.

Aliitaja miradi mingine kuwa ni Ujenzi wa tanki la kihifadhia maji la lita 100,000 katika eneo la Ulowa Na.1, Ujenzi wa vituo 35 vya kuchotea maji (DPs), Ununuzi wa vifaa kwa ajili ya kuunganishia wateja 1,000 wa majumbani, Ujenzi wa jengo la ofisi litakalotumiwa na Chombo cha Watoa Huduma ya Maji Ngazi ya Jamii (CBWSO), Ujenzi wa jengo kwa ajili ya kutibu maji, Ununuzi wa Magari mawili (2) aina Toyota hardtop na Double cabin kwa ajili ya usimamizi na ufuatilaiji wa mradi, Ununuzi wa Pikipiki 2 kwa ajili ya usimamizi na ufuatilaiji wa mradi Ununuzi wa sanduku la vitendea kazi (Tool box), na Ununuzi wa mashine ya kuunganishia bomba za HDPE Ukubwa wa kuanzia milimita 40 hadi milimita 200.

Naye Mbunge wa Jimbo la Ushetu Mhe Dkt. Emmanuel Cherehani alisema kuwa kwa ujumla mradi huo utahudumia watu takribani 189,836 wa Kata za Igunda, Kisuke, Kinamapula,Nyamilangano, Mapamba,Uyogo,Bukomela,Ushetu na Ulowa.

Share: