Mwanadada kutoka Uingereza afariki dunia kwa kutumia vidonge vya kupunguza uzito wa mwili

Vifo vinavyotokana na urembo pamoja na harakati za kupunguza mwili vimeendelea kuripotiwa Duniani ambapo mwingine ambaye amepoteza uhai kwa kujaribu kupunguza uzito wa mwili wake ni Mwanamke wa Uingereza aitwae Sarah Thompson, Mama wa Watoto wawili ambaye kifo chake kimesababishwa na kutumia vidonge vya kupunguza uzito ambavyo aliviweka chini ya ulimi kwa lengo la kupunguza kilo.

Sarah aliyewahi kupambana na Saratani ya koo alipata changamoto za uzito baada ya matibabu yake na kutokana na hali hiyo aliazimia kupunguza uzito ambapo ndani ya mwezi mmoja alishuka kutoka kilo 98 hadi 70 lakini hata hivyo Familia yake imesema dawa hizo zilisababisha athari mbaya ikiwa ni pamoja na kichefuchefu na kushindwa kula hali iliyopelekea kifo chake.

Mkemia alithibitisha kuwa dawa hizo zilikutwa na kemikali hatari iitwayo Clenbuterol ambayo ni dawa ya kudhibiti pumu kwa Farasi lakini pia hutumiwa vibaya kwa ajili ya kupunguza mafuta mwilini na athari za dawa hiyo ni pamoja na shinikizo la moyo na kichefuchefu, Gabriella Dada wa Marehemu naye alisimulia jinsi alipojaribu kutumia dawa hizo alikumbwa na mapigo ya haraka ya moyo na maumivu makali na hivyo kuamua kuachana nazo mara moja.

Polisi walithibitisha kupokea taarifa ya kifo hicho na wamepeleka nyaraka zote kwa Mkaguzi wa Maiti ili kufanikisha uchunguzi zaidi huku Serikali ya Uingereza ikiahidi kuchukua hatua za kuzuia matumizi mabaya ya Madawa kwa afya ya umma.

Share: