
Mwanamume anayeshutumiwa kwa kumpiga risasi Charlie Kirk amekiri kumuua mwanaharakati huyo wa mrengo wa kulia katika ujumbe aliomuandikia mpenzi wake, waendesha mashitaka wamedai, huku wakitangaza mashtaka saba dhidi yake.
Tyler Robinson, 22, aliacha barua chini ya baobonye ili mwenzake ajue alichofanya, alisema Wakili wa Kaunti ya Utah Jeffrey Gray akiongeza kuwa mwenzake huyo alikuwa mpenzi wa mshtakiwa.
Kulingana na Bw Gray, barua hiyo ilisema: "Nilipata fursa ya kumuondoa Charlie Kirk, na nimeitumia."
Mwendesha mashtaka pia alituma ujumbe wa maandishi kati ya wawili hao ikiwa ni pamoja na mmoja ambao mshtakiwa alisema kuwa alimpiga risasi Kirk kwa sababu "namchukia sana".
Mshukiwa anazuiliwa bila dhamana katika kitengo maalum cha makazi katika jela ya kaunti ya Utah. Alifikishwa mahakamani kwa mara ya kwanza Jumanne, huku waendesha mashtaka wakisoma mashtaka saba dhidi yake.
Mashitaka hayo ni mauaji ya kuchochewa, kukutwa na silaha, makosa mawili ya kuzuia haki, makosa mawili ya kuharibu ushahidi, na kufanya uhalifu wa kutumia nguvu wakati watoto wapo.