
Mshukiwa wa mauaji ya mwanasiasa mashuhuri wa Ukraine Andriy Parubiy amekamatwa, Rais wa nchi hiyo Volodymyr Zelensky amesema.
Mbunge huyo mwenye umri wa miaka 54 aliuawa na mshambuliaji aliyejifanya mjumbe katika mji wa magharibi wa Lviv siku ya Jumamosi, na kusababisha msako mkali.
Waziri wa mambo ya ndani wa Ukraine Igor Klymenko alisema katika taarifa yake aliyoitoa alfajiri ya Jumatatu kwamba mshukiwa amezuiliwa katika eneo la Khmelnytskyi magharibi.
Parubiy alipata umaarufu wakati wa maandamano makubwa ya Ukraine ya Euromaidan, ambayo yalitetea uhusiano wa karibu na EU na kumwangusha Rais wa zamani wa Urusi Viktor Yanukovych mnamo 2014.
Klymenko alisema uchunguzi wa awali umegundua mauaji hayo "yalipangwa kwa makini" na kuzingatia ratiba ya safari ya Parubiy na njia ikapangwa pamoja na mpango wa kutoroka.
Aliongeza kuwa jeshi la polisi la taifa la Ukraine litatoa maelezo zaidi baadaye.
Katika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii, Zelensky alisema alikuwa amezungumza na mwendesha mashtaka mkuu Ruslan Kravchenko ambaye alisema kwamba mshukiwa ametoa ushahidi wa awali.