Mshauri wa usalama wa taifa wa marekani afanya mazungumzo saudi arabia

Mshauri wa usalama wa taifa wa Marekani Jake Sullivan amefanya mazungumzo na Mwanamfalme wa Saudia Mohammed bin Salman alipotembelea Saudi Arabia.

Majadiliano yalilenga kuhusu vita vya Israel-Gaza na masuala mengine ya kikanda, ikiwa ni pamoja na juhudi za kuzuia mashambulizi ya Houthi dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari Nyekundu.

Shirika la habari la Reuters linamnukuu afisa mmoja akisema wawili hao walijadili juhudi za "kudumisha utulivu katika eneo lote na kuzuia mzozo wa Israel na Hamas kuenea".

Afisa huyo anaongeza kuwa Sullivan alilenga kuendeleza kazi ambayo tayari inaendelea ili kujaribu kuleta amani endelevu kati ya Waisraeli na Wapalestina.

Mshauri huyo wa usalama wa taifa sasa anatarajiwa kusafiri hadi Israel, ambako atarajiwa kufanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na wajumbe wa baraza la mawaziri la vita.

Share: