Miaka kumi tangu kupotea kwa ndege ya malaysia iliyokuwa na abiria 227

Leo Machi 8 ni miaka kumi kamili tangu kupotea kwa ndege ya serikali ya Malaysia aina ya Boeng 777 ikiwa na abiria 227 na wahudumu wa ndege 12.

Majira ya usiku ndege hiyo ilikuwa ikitokea Kuala Lumpur kwenda Beijing China na ikiwa imekaribia kuingia Vietnam, ndege hiyo ghafla ilibadili mwelekeo na mawasiliano yote ya kielektroniki yalikatika.

Ilirudi nyuma kurudi Malaysia kulingana na rada za kijeshi za Malaysia na Thailand na kisha ikaelekea kusini mwa bahari ya Hindi, nadharia za wakati huo zikiwa ni kwamba huenda ndege hiyo iliishiwa mafuta ikiwa angani.

Operesheni kubwa na za gharama zimefanyika kufikia leo zikilenga kwenye utafutaji na hakuna mtu yeyote aliyewahi kupatikana miongoni mwa waliokuwa kwenye ndege hiyo.

Maelfu ya wataalamu wa masuala ya bahari, wahandisi wa anga na mafundi kadhaa walitumia taarifa za mwisho za ndege hiyo bila kupata majibu ya ilipoishia safari ya ndege hiyo.

Baadhi ya mabaki ya ndege hiyo inaelezwa kuwa yalipatikana zaidi ya miezi 16 baadae mengi yakipatikana kwenye fukwe ya bahari ya Hindi hasa upande wa Afrika mashariki.

Kuna nadharia nyingine kuwa kila mtu kwenye ndege hiyo alizimia kutokana na ukosefu wa oksijeni baada ya mfadhaiko usioeleweka au janga la moto ama mlipuko wa ghafla uliokata mawasiliano.

Serikali ya Malaysia tayari imefufua msako mwingine wa kuitafuta ndege hiyo suala ambalo limerejesha matumaini ya maelfu ya watu waliopoteza ndugu zao kwenye mkasa huo.

Share: