Mhe.kikwete asikitishwa na wimbi kubwa la watumishi wanaotaka kuhama halmashauri ya kilolo

Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe.Ridhiwani Kikwete amesikitishwa na wimbi kubwa la wafanyakazi hususan walimu wanaotuma maombi ya kutaka kuhama katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilolo, Mkoani Iringa.

Mhe.Kikwete ametoa kauli hiyo wakati akizungumza na Watumishi wa Halmashuuri ya Kilolo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake ya kikazi Mkoani humo ya kuzungumza na kusikiliza kero za watumishi na kuzitafutia ufumbuzi.

Amesema Watumishi walio wengi wanaotaka kuhama wamekuwa wakitaja sababu zinazofanana jambo ambalo lina walakini huku akisema kuna matatizo ya kiuongozi katika Halmashauri hiyo .

Ametaja moja ya sababu zinazopelekea Watumishi hao kutaka kuhama ni pamoja na kupuuzwa na kutokusikilizwa pindi watumshi hao wanapokuwa na changamoto.

Amefafanua kuwa katika Halmashauri hiyo Maafisa Utumishi na Maafisa Tawala wamekuwa miungu watu badala ya kuwa suluhisho la matatizo yanayowakabili watimishi wanaowasimamia.

Amesema licha ya watumishi wengi wanaotaka kuhama kutaja sababu inayofanana, kuwa ni uwepo wa baridi kali na hivyo kusumbuliwa na "athma" jambo ambalo si kweli, ukweli ni kwamba hakuna mahusiano mazuri kati ya Watumishi na Uongozi wa Halmashauri hiyo.

Kufuatia hatua hiyo Mhe.Kikwete amemtaka Mkurugenzi kufanyia kazi changamoto zinazowakabili watumishi hao ikiwemo kufanya vikao vya mara kwa mara na watumishi kwa ajili ya kuwasikiliza pamoja na kuzingatia stahili zao ikiwepo posho za likizo.

Share: