Mhe. pindi chana(mb.) ameipongeza rwanda kwenye maadhimisho ya miaka 30 ya mauaji ya kimbari

Mhe. Pindi Chana(Mb.), Waziri wa Katiba na Sheria amemwakilisha Mhe. January Y. Makamba(Mb.), Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kwenye maadhimisho ya Miaka 30 ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda yaliyofanyika leo tarehe 7 Aprili kwenye Ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam. 

Katika hotuba yake, Mhe. Waziri Chana alikumbusha jinsi Tanzania ilivyoshuhudia mauaji hayo na namna Watanzania walivyoopoa miili ya wahanga katika Mto Kagera na kuzika kwenye Kaburi la pamoja lililopo Rusumo, wilayani Ngara, mkoani Kagera.

Aliipongeza Rwanda kwa mafanikio makubwa iliyopata katika kipindi cha miaka 30 tangu kutokea kwa mauaji hayo.

Alitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutoruhusu tena kilichotokea nchini Rwanda kisitokee mahali kwingine kwa kudhibiti na kuchukua hatua dhidi ya viashiria vya chuki katika jamii.

Mwisho, Mhe. Waziri Chana alisema kuwa Tanzania na Rwanda ni ndugu sio tu kwasababu ya mpaka bali pia uhusiano wa karibu na kihistoria uliopo kati ya wananchi wa mataifa hayo mawili.

Share: