Mbelwa Kairuki: HKMU, KPIL na hospitali ya Kairuki zisingekuwepo Bila Mzee mwinyi

Balozi wa Tanzania Nchini Uingereza Mbelwa Kairuki amesema Watu wengi wamemuelezea vizuri Hayati Mzee Mwinyi jinsi alivyokuwa Jasiri, Mnyenyekevu, Muungwana, Mzazi na Mlezi na alivyofanya mageuzi ya kiuchumi na kufungua Nchi huku akisema mfano mmoja ni namna alivyotoa kibali cha kufunguliwa Hospitali Binafsi ya TAG Mikocheni Hospital (ambayo hivi sasa inajulikana kama Kairuki Hospital).

“Marehemu Prof. Hubert Kairuki alipata wazo la kuanzisha Hospitali katika miaka ya 80 kipindi ambacho Sheria ilikuwa hairuhusu watu binafsi kuanzisha hospitali isipokuwa taasisi za dini, Prof Kairuki aliamua kushirikiana na Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) ili kufanikisha azma hiyo, hata hivyo Watendaji ndani ya Wizara ya Afya waliokuwepo wakati huo walimshawishi Waziri wa Afya aliyekuwepo wakati huo asikubali kutoa kibali na huo ndio ulikuwa ni uamuzi wa mwisho wa Waziri hakutaka kusikiliza habari ya Hospitali hiyo”

“Mzee Mwinyi alipata taarifa ya changamoto hiyo kutoka kwa Mpambe wake (ADC) Marehemu Colonel Thabit, baada ya kusikia habari hiyo Mzee Mwinyi alimuita Marehemu Prof Kairuki na kumtaka amsimulie yaliyomsibu, baada ya kusikiliza, Mzee Mwinyi alitoa idhini mwenyewe kwamba Hospitali ifunguliwe na akamuagiza Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Marehemu Hemed Mkali akaifungue kwani watu wa Wizara ya Afya walikuwa na kinyongo, shughuli hiyo ilifanyika tarehe 17 Machi 1987” Balozi Mbwela

“Sina shaka kwamba, kama sio Mzee Mwinyi kufanya uamuzi ule, leo hii Kairuki Hospital na taasisi nyingine kama HKMU, KPIL zisingekuwepo, funzo kubwa alilotuachia Mzee wetu Ali Hassan Mwinyi hususan wenye dhamana za kutumikia wananchi katika ngazi mbalimbali tunapaswa kuwa na usikivu, unyenyekevu na kutenda haki, ubabe, umaarufu binafsi wa muda mfupi sio sifa nzuri na za kudumu kwa Mtumishi wa umma, Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Hayati Mheshimiwa Rais Ali Hassan Mwinyi Mahala Pema Peponi, AMEN” Balozi Mbwela.

Share: