Marekani yawashambulia wanamgambo wanaoungwa mkono na iran nchini iraq

Jeshi la Marekani limeshambulia vikundi vya wanamgambo wanaoungwa mkono na Iran nchini Iraq, saa chache baada ya wafanyakazi wa Marekani kujeruhiwa katika shambulio la ndege zisizo na rubani kwenye kambi ya anga ya Marekani huko.

Mkuu huyo wa ulinzi wa Marekani alisema maeneo matatu yanayotumiwa na Kataib Hezbollah na makundi mengine yalipigwa kujibu mashambulizi dhidi ya vikosi vya Marekani nchini Iraq na Syria.

Mashambulizi ya Marekani yalilaaniwa na Iraq kama "kitendo cha wazi cha uadui".

Marekani imekuwa ikilenga mara kwa mara maeneo yanayohusishwa na makundi ya wapiganaji nchini Iraq na Syria katika miaka ya hivi karibuni.

Iraq inasema mtu mmoja aliuawa na wengine 18 wakiwemo raia wamejeruhiwa katika mashambulizi ya Marekani.

Waziri wa Ulinzi Lloyd Austin alisema mashambulizi hayo, ambayo aliyaita "ya lazima na sawia", yameidhinishwa na Rais Joe Biden.

Msemaji wa Baraza la Usalama la Kitaifa la Marekani Adrienne Watson amesema shambulizi la ndege zisizo na rubani katika kambi ya Marekani huko Irbil katika eneo la Kurdistan nchini Iraq limewajeruhi wanajeshi watatu wa Marekani.

Kundi la wanamgambo linaloitwa Islamic Resistance in Iraq, lenye uhusiano na Kataib Hezbollah, lilisema ndilo lililohusika na shambulio hilo. Kambi ya anga ya Irbil hapo awali ilishambuliwa na mashambulizi ya roketi yaliyofanywa na wanamgambo wenye uhusiano na Iran.

Kataib Hezbollah, ambayo inafadhiliwa na kumiliki silaha na Iran, imekuwa moja ya makundi mashuhuri yaliyohusika katika mashambulizi dhidi ya shabaha za Marekani nchini Iraq.

Share: