Marekani yapinga wito wa kimataifa wa kusitisha mapigano israel gaza

Marekani imekataa wito wa kimataifa wa kusitisha mapigano kati ya Israel na kundi la Palestina Hamas, ikisema kuwa si "jibu sahihi hivi sasa.

Msemaji wa Usalama wa Kitaifa John Kirby alitoa maoni hayo siku ya Jumatatu, akipendekeza badala yake "kusitisha" mapigano kwa muda ili kuruhusu msaada kuwasilishwa ndani ya Gaza.

Hivi sasa, usambazaji wa chakula, maji, mafuta na madawa kwa wakazi milioni 2.2 wa Gaza uko chini sana. Lakini Israel imeapa kuwa hakutakuwa na usitishaji mapigano hadi Hamas itakaposambaratishwa.

"Miito ya kusitishwa kwa mapigano ni wito kwa Israel kujisalimisha kwa Hamas, kujisalimisha kwa ugaidi...hili halitafanyika," Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema.

Akizungumza katika kikao na wanahabari, Bw Kirby alisema ana imani malori zaidi ya misaada yataweza kuingia Gaza kupitia Misri.

Alisema Marekani imezungumza na serikali ya Israel kuhusu kuongeza idadi ya lori zinazovuka mpaka kila siku hadi karibu 100, Takriban malori 45 yalikuwa yameingia Gaza kupitia kivuko cha Rafah nchini Misri siku ya Jumapili, Bw Kirby alisema. Lakini, alikubali zaidi ingehitajika.

"Tunajua kwamba hata hiyo, ambayo ni uboreshaji mkubwa juu ya tulipo hivi sasa, bado haitatosha," aliambia mkutano wa waandishi wa habari.

Philippe Lazzarini, kamishna mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada UNRWA, awali aliambia BBC kwamba takriban lori 500 kwa siku zilikuwa zikiingia Gaza kabla ya vita kuanza.

Israel imekuwa ikishambulia kwa mabomu Gaza tangu mashambulio ya Oktoba 7 ya Hamas yaliyoua watu 1,400 nchini Israel na kuona watu 229 wakichukuliwa mateka na Hamas.

Zaidi ya watu 8,300 huko Gaza wameuawa tangu mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel yaanze, kulingana na wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas.

Yinam Cohen, balozi mdogo wa Israel katika eneo la Midwest, alisema siku ya Jumatatu kuwa mwanamke mmoja alishikiliwa mateka na Hamas; Natalie Raanan, alikuwa amerejea nyumbani Chicago.

Wiki iliyopita, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilitoa mwito wa kusitishwa mara moja kwa mapatano ya kibinadamu kati ya Israel na Hamas, ambayo yalitupiliwa mbali kwa hasira na Israel.

Siku ya Jumatatu, Bw Lazzarini alisema mfumo wa kutoa msaada "utashindwa isipokuwa kutakuwa na dhamira ya kisiasa ya kufanya mtiririko wa vifaa kuwa wa maana, unaolingana na mahitaji ya kibinadamu ambayo hayajawahi kushuhudiwa".

Israel ilianza kile Bw Netanyahu alichokiita "hatua ya pili" ya vita vilivyonuiwa kuangamiza Hamas siku ya Jumatatu, huku vikosi vya ardhini vikipanua operesheni zao ndani ya Gaza baada ya wiki tatu za mashambulizi makali ya mabomu.

Majeshi ya Israel yameingia zaidi kaskazini mwa Ukanda wa Gaza, huku vifaru vikikata kwa muda njia ya kuwahamisha watu kuelekea kusini, mashahidi wa Palestina wanasema.

Kifaru kimoja kilirekodiwa kwenye picha ya video kwenye Barabara ya Salah al-Din, na hivyo kuzua uvumi kuwa inaweza kuwa sehemu ya vikosi vya mwanzo kwenye Jiji la Gaza.

Video ilionyesha gari likigeuka nyuma baada ya kukaribia kifaru ambacho kinaonekana kufyatua risasi na kuliharibu.

Baadaye, jeshi la Israel lilisema mwanajeshi aliyekuwa akishikiliwa mateka na Hamas aliokolewa katika operesheni ya usiku ya kuamkia leo.

Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alipongeza kuachiliwa kwa Pte Ori Megidish, ambaye alisemekana kuwa "anaendelea vyema", kama "mafanikio ya kusisimua" ambayo yalionyesha kujitolea kwa Israeli kuwaachilia mateka wengine zaidi ya 230.

Pia alilaani kama "propaganda za kikatili za kisaikolojia" video iliyotolewa na Hamas ambayo ilionyesha wanawake wengine watatu wa Kiisraeli wakiwa utumwani huko Gaza wakitaka akubali kubadilishana wafungwa.

Mateka hao - ambao ni pamoja na makumi ya watoto na wazee, pamoja na wanajeshi - walichukuliwa na watu wenye silaha wa Hamas wakati wa shambulio ambalo halijawahi kushuhudiwa kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba ambapo watu 1,400 waliuawa.

Mwishoni mwa juma, Israel ilianza kile Bw Netanyahu alichoita "hatua ya pili" ya vita vinavyonuiwa kuangamiza Hamas, huku vikosi vya ardhini vikipanua operesheni zao ndani ya Gaza baada ya wiki tatu za mashambulizi makali ya mabomu.

Wizara ya afya ya Gaza inayoendeshwa na Hamas inasema zaidi ya watu 8,300 wameuawa katika eneo hilo tangu wakati huo, huku usambazaji wa chakula, maji, mafuta na dawa kwa wakazi wake milioni 2.2 ukiwa mdogo.

Bw Netanyahu pia amekataa wito wa kusitishwa kwa mapigano huko Gaza, akisema kuwa kusitisha operesheni za kijeshi itakuwa "kujisalimisha kwa Hamas, kusalimu amri kwa ugaidi, kusalimu amri kwa unyama".

"Leo tunaweka mstari kati ya nguvu za ustaarabu na nguvu za kishenzi," aliambia mkutano wa wanahabari siku ya Jumatatu. "Israel itasimama dhidi ya nguvu za kishenzi hadi ushindi. Natumai na kuomba kwamba mataifa yaliyostaarabika kila mahali yataunga mkono vita hivi."

Mashirika ya misaada yametoa wito mara kwa mara kusitishwa kwa mapigano ili kupeleka misaada katika eneo lililozingirwa.

Share: