sheria zinazuia watumishi wa umma kutumia magari ya Serikali kwa matumizi binafsi
Serikali imesema magari yote ya Serikali yanatakiwa kuwa yameegeshwa sehemu zilizotengwa kwa ajili hiyo ifikapo saa 12:00 jioni bila kukosa, vinginevyo kiwepo kibali maalum.
Naibu Waziri wa Ujenzi Godfrey Kasekenya amesema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Jimbo Arumeru Magharibi, Noah Saputu aliyeuliza ni lini Serikali itazuia kupaki magari ya Serikali sehemu za starehe baada ya saa za kazi.
"Tunawakumbusha na kuwasisitiza maafisa na waajiri wote sheria zimeelekeza mtumishi yeyote anayemiliki chombo cha umma na hasa magari asiwe barabarani baada ya saa 12 jioni na asiweze kuwa katika maeneo ambayo si sahihi (maeneo ya starehe) kwa muda ambao hauruhusiwi," ameongeza Kasekenya wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Jimbo la Makete, Festo Sanga.
Hata hivyo Kasekenya amesema sheria zinazuia watumishi wa umma kutumia magari ya Serikali kwa matumizi binafsi na kuagiza kwa wale watakaokwenda kinyume watachukuliwa hatua za kinidhamu.