Madaktari bingwa wa Rais Samia tumekufikia, karibu tukuhudumie
Madaktari bingwa 35 wa magonjwa mbalimbali wamewasili mkoani Arusha leo Mei 20,2024, wakitarajiwa kutoa huduma za matibabu na ushauri kwa gharama nafuu kwa wakazi wa mkoa wa Arusha kwa siku tano mfululizo kwenye hospitali zote za wilaya za Mkoa wa Arusha.
Hospitali zinazotarajiwa kuhudumiwa na madaktari hawa bingwa maarufu kama Madaktari wa Samia ni Hospitali ya Jiji la Arusha, Hospitali ya wilaya ya Longido, Hospitali ya wilaya ya Monduli na Hospitali ya wilaya ya Meru.
Hospitali nyingine ni Hospitali ya wilaya ya Karatu, Hospitali ya Olturumet Halmashauri ya Arusha na Hospitali ya wilaya ya Ngorongoro ambapo huduma mbalimbali zinatarajiwa kutolewa ikiwemo huduma ya afya ya uzazi na afya kwa watoto,huduma za upasuaji na huduma za magonjwa ya ndani ikiwemo shinikizo la damu, kisukari pamoja na huduma za ganzi na usingizi.
Joachim Mashunga ambaye ni Afisa mradi kutoka Wizara ya afya amewaalika wananchi wote wa Arusha kujitokeza kwa wingi kwenyw hospitali za Wilaya akisema kuwa huduma hizo za matibabu zinawasaidia wananchi kuondokana na gharama za kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kibingwa kwenye hospitali za mkoa.
Naye Dkt. Charles Mkombachepa ambaye ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Arusha na Dkt. Emeliaba Mvungi, daktari bingwa wa afya ya uzazi na kizazi wanasema madaktari hao pia wanatoa fursa ya kuwajenge uwezo madaktari wenyeji ili kuweza kuwahudumia wananchi kikamilifu.
Ujumbe wa madaktari hao bingwa wa magonjwa mbalimbali wanaohudumia wananchi wa Arusha unasema "Madaktari bingwa wa Rais Samia tumekufikia, karibu tukuhudumie."